SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imewatoa hofu Mfuko wa Hifadhi ya Huduma za Jamii Zanzibar, (ZSSF) na kuwataka kuwekeza fedha zao kwenye miradi mikubwa ya Serikali ya kimakakati.Pia, Serikali imejizatiti kuweka dhamana ya miradi mikubwa ya maendeleo itakayotekelezwa na Mfuko huo pamoja na kuwahakikishia usalama wa fedha zao endapo zitaathiriwa kwa namna yoyote na ujenzi wa miradi hiyo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, aliyasema hayo alipoweka jiwe la msingi la ujenzi wa maegesho ya magari, Malindi Wilaya ya mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.Alisema, lengo la Serikali kuweka ujenzi wa maegesho hayo ni kupunguza msongamano wa magari mjini pamoja na kuweka usafiri wa umma wa aina moja na wa kisasa ili kwenda sambamba na mahitaji ya mji kwa wakati uliopo.
Alisema, hayo ni maegesho ya kwanza ya ghorofa kujengwa Zanzibar, yenye hadhi na mitambo ya kisasa.Rais Dk. Mwinyi alitoa ushuhuda wa Mifuko ya hifadhi ya Jamii kwa mataifa mengine duniani ikiwemo Indoneia na Malaysia yamejenga nchi zao kwa kuweka miundominu ya kisasa, miji mikubwa, maduka, barabara na madaraja makubwa ya maendeleo, hivyo aliwatoa wasiwasi ZSSF na kuwataka kuiga mifano ya mataifa hayo kwa kuijenga upya Zanzibar bila kujali hasara ya fedha zao kwani Serikali imewapa dhamana ya fedha hizo.
Alisema, Serikali pia imepanga kuweka vituo vikuu viwili vya mabasi ya umma kwa maeneo ya Kijangwani na Malindi ili kukidhi hadhi ya mji yenye kwenda sambamba na maendeleo ya mataifa mengine duniani.Akizungumzia athari zinazoathiri Hifadhi ya Taifa ya Mji MKongwe wa Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi amesema ujenzi wa maegesho hayo umezingatia na kufuata taratibu zote zilizowekwa na hifadhi hiyo kwa mujibu wa matakwa ya UNESCO juu ya mabadiliko ya maendeleo yanayotekelezwa kwenye maeneo ya Mji Mkongwe.
Aidha, Dk. Mwinyi alieleza, maegesho hayo yatapunguza msongamano maeneo ya Darajani na Mji Mkongwe kwa kutoruhusu baadhi ya vyombo vya usafiri kuingia kwenye hifadhi ya mji Mkongwe ili kuunusuru mji huo na athari ya vyombo hivyo.Akizungumzia athari kwa Hifadhi ya Taifa ya Mji MKongwe wa Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi amesema ujenzi wa maegesho hayo umezingatia na kufuata taratibu zote zilizowekwa na hifadhi hiyo kwa mujibu wa matakwa ya UNESCO.
Kuhusu mazingira ya wafanyabiashara wa maeneo ya mjini (Darajani), Dk. Mwinyi alieleza Serikali imekusudia kujenga eneo maalumu la wafanyabiashara hao lenye hadhi ya juu na mwonekano wa kisasa, ili kuepusha wafanyabiashara kuenea kiholela barabarani na kueleza kuwa eneo la Darajani ni kitovu kikuu cha biashara, Zanzibar.
Alisema, ujenzi huo pia utahusisha barabara kuu ya Darajani pamoja na eneo maalum la wafanyabiasha.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohammed, alisema juhudi za Mapinduzi zinazoendelezwa na awamu ya nane ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni mapinduzi ya Uchumi na kuboreshwa maendeleo kwa kuendelezwa miradi mikubwa ya maendeleo kwenye sekta zote za jamii ikiwemo Afya, elimu, sekta ya miundombinu na Barabara, maji safi, makaazi ya kisasa ya wananchi na viwanja vya michezo vyenye hadhi ya kimataifa.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Aboud Hassan Mwinyi, alisema ujenzi wa maegesho hayo unatarajiwa kuchukua gari 200 kwa wakati mmoja, utagharimu bilioni 6.83 hadi kukamilika kwake na sasa umefikia asilimia 65 ya ujenzi wote.Pia, alisema ujenzi huo umetoa ajira kwa wazawa ikiwemo wakandarasi wasaidizi pamoja na Serikali kukusanya mapato yanayotokana na ujenzi huo.
Mapema akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), Nassor Shaaban Ameir alisema mbali na mradi huo wa maegesho ya magari ya ghorofa, Malindi pia wanatarajia kuanza ujenzi mwengine wa kituo kikubwa cha mabasi ya uma kwenye eneo hilo.