Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema, Zanzibar imefungua milango wazi kwa fursa za biashara na uwekezaji na tayari imewakaribisha wadau mbalimbali kushirikiana nao kwenye maono ya ukuaji wa Uchumi endelevu na ustawi wa utalii wa muda mrefu.

Rais Dk.Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 25 Oktoba 2024 alipofungua maonesho ya Utalii na Uwekezaji Zanzibar, 2024 huko viwanja vya maonesho ya Biashara Nyamanzi Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Aidha Rais Dk.Mwinyi amesema Serikali itaendelea kukuza mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji pamoja na kuweka mkazo wa kurahisisha michakato, kuimarisha mifumo ya udhibiti na kutoa motisha za kuvutia uwekezaji nchini.

Rais Dk. Mwinyi aliwashauri wadau wa Utalii kuendeleza utamaduni na shauku ya kufanya Maonesho ya Utalii na Uwekezaji si kwa mnasaba wa Zanzibar pekee bali kwa Afrika

Mashariki na medani za kimataifa ili kuendelea kuitangaza nchi na vivutio vyake duniani kote.
Halikadhalika Rais Dk. Mwinyi alibainisha kwamba faida za utalii na uwekezaji zinufaishe visiwa vyote vya Unguja na Pemba kwa kutengeneza fursa kwa watu wote.

Maonesho hayo ya Utalii na uwekezaji Zanzibar, 2024 yameandaliwa kwa ushirikiano baina Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, Kamisheni ya Utalii, na sekta binafsi.

Katika hafla hiyo pia kulisainiwa makubaliano ya Ushirikiano baina ya Kamisheni ya Utalii Zanzibar na Mamlaka ya Uwekezaji na vitega Uchumi, ZIPA katika kuendeleza kazi za utalii na kurahisisha uwekezaji kwa kuendeleza vivutio vipya kwa maeneo ya utalii nchini na makubaliano baina ya Kamisheni ya Utalii Zanzibar na Baraza la Sanaa Zanzibar katika kuondosha changamoto zinazotokana na utalii, hususan eneo muziki, sanaa na burudani.