RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuanzia sasa Serikali itawafidia nyumba bora wananchi wanaotoa maeneo yao kupisha miradi ya maendeleo.Rais Dk. Mwinyi amefahamisha kuwa Serikali imedhamiria na jukumu la msingi la kuhakikisha wananchi wanapata makaazi bora ya kuishi.Ameeleza kuwa kumekuwa na baadhi ya wananchi wanazoendelea kujenga nyumba zisizo na ubora (Vibanda) licha ya kufidiwa fedha za kutosha na Serikali.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo, alipozindua Mradi wa mauzo wa Nyumba za Chumbuni zinazojengwa na Shirika la Nyumba, Zanzibar Ukumbi wa Mikutano Hoteil ya Amani, Mkoa wa Mjini Magharibi.Rais Dk. Mwinyi amefahamisha kuwa jitihada hizo zimekuwa endelevu kwa awamu tofauti zilizoanza baada ya Mapinduzi ya Januari 1964 Chini ya Uongozi wa Hayati Abeid Aman Karume.
Dk. Mwinyi amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kutafuta fedha zaidi za kuuendeleza Miradi mikubwa ya Ujenzi wa Nyumba za Maakazi maeneo mbalimbali.Aidha Rais Dk. Mwinyi amezisitiza taasisi za kifedha ziliopo kufanya kazi kwa ukaribu na Shirika la nyumba la Zanzibar ili kufanikisha azma hiyo. Amefahamisha kuwa Ujenzi wa Nyumba Bora za Makaazi unaenda Sambamba na Uimarishaji wa Miji Bora na Barabara zitakazotoa taswira nzuri ya Nchi.
Halikadhalika, Rais Dk. Mwinyi ametoa rai kwa Wananchi kuhamasika kununua nyumba hizo ili kuwa na Makaazi bora na ya kisasa.Hata hivyo, Dk. Mwinyi amelisisitiza Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC)kuendelea kutafuta Soko la Nyumba zinazojengwa kwani ni wajibu pamoja na kuwa na Nyumba nyengine za kuwakodisha wananchi.Rais Dk ,Mwinyi amefahamisha kuwa ni vyema kwa wananchi kununua nyumba hizo hivi sasa kwa maeneo yanayojengwa yatakuwa na biashara nyingi baadae Pamoja na shughuli za kijamii na barabara za uhakika.
Ameishauri taasisi kutoka Sekta Binafsi kushirikiana na Shirika la Nyumba ili lipate mafanikio zaidi.Rais Dk. Mwinyi pia ameipongeza taasisi ya Infinity Group of Companies kwa wazo la kuwekeza Zanzibar na mpango wao wa kuwajengea uwezo Vijana wa Zanzibar kwenda kujifunza nchini Dubai ili kuleta uzoefu huo Zanzibar.
Rais Dk Mwinyi ameeleza kufarijika na kasi ya Utendaji wa Shirika la Nyumba hivi sasa kwani limekuwa likitekeleza Miradi yenye tija badala ya kushughulikia Migogoro ya Nyumba kwa Muda mrefu. Pia, ametumia fursa hiyo kuwahimiza Watendaji wa Sekta ya Umma wanaokabidhiwa Majukumu kuhakikisha Wanaacha Alama katika maeneo yao ya kazi yatakayowajengea heshima wakati wote.
Akitoa Taarifa ya Kitaalamu ya Mradi huo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzbar, Sultan Said ameeleza kuwa Mradi huo ni Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020-2025 ya kuimarisha nyumba za Makaazi.Ameeleza Mradi wa Chumbuni Utakuwa na Nyumba 3000 na Shirika linakusudia kuuendeleza Miradi mikubwa ya Kimkakati ya Ujenzi wa Nyuma maeneo ya Kikwajuni, Kwa Mchina Unguja, Kisakasaka na Mabaoni Mfikiwa Pemba.
Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi, Rahma Kassim Ali ameleza kuwa kuanzishwa Idara ya Maendeleo ya Makaazi kutaleta chachu ya utekelezaji wa Sera ya Makaazi itakayoleta Mafanikio makubwa hapo baadae.Amebainisha kuwa Wizara bado ina maeneo mengi yaliotengwa kwa ajili ya Maendeleo ya Makaazi ili kufanikisha dhamira ya Serikali ya kuwa na Miji Bora.