SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema imeweka uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya Afya kutokana na umuhimu wa sekta hiyo kwa jamii.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na Meneja Mwandamizi wa Mfuko wa dunia (Global Fund), Dk. Sara Asiimwe na ujumbe wake ulioongozwa na Waziri wa Afya, Nassor Ahmed Mazrui.

Ameishukuru “Global Fund” kwa jitihada zake za kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuisaidia kwenye masuala mbalimbali ya Maendeleo ikiwemo Sekta ya Afya.Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameeleza juhudi za “Global Fund” kuisaidia Zanzibar kwenye sekta ya Afya na nyengine za maendeleo ni kuendeleza jitihada za Serikali anayoiongoza katika kutekeleza adhma ya Serikali kutoa huduma bora za afya.

Akizungumzia huduma ya bima ya Afya kwa wageni wanaoingia Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi, ameieleza “Global Fund” dhamira ya Serikali kuja na bima hiyo kutokana na umuhimu wake kwa wageni, hivyo ameuomba Mfuko huo kuangalia namna ya kuiungamkono Serikali.

Pia, Dk. Mwinyi amepongeza Ushirikiano uliopo baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na “Global Fund” hasa kufanyakazi kwa karibu na Wizara ya Afya kwenye mradi wa kuzalisha Hewa Tiba (Oxegen Plant) kwenye hospitali ya Rufaa ya Lumumba.

Naye, Dk. Sara Asiimwe alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba “Global Fund” inafanyakazi kwa karibu zaidi na Serikali ya Mapnduzi ya kupitia Sekta zake za Maendeleo ikiwemo Wizara ya Afya. Aidha, aliiahidi Serikali kwamba taasisi yao itaendeleza ushirikiano wake na Zanzibar hasa kwenye miradi ya maendeleo.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Waziri wa Afya, Nassor Ahmed Mazrui, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, kitengo cha (ZGFCCM), inafanyakazi kwa karibu na Mfuko wa Dunia, (Global Fund) hasa katika kupambana na Malaria, UKIMWI na Kifua Kikuu.Amesema, tokea kuanzishwa kwake Global Fund mwaka 2002 imekua mdau wa karibu kuiungamkono Serikali kupitia Sekta ya Afya na miradi mengine ya Maendeleo.

Ameeleza Wizara ya Afya kwa kushirikiana na “Global Fund” wamefanya uwekezaji mkubwa wa kuweka mtambo wa kuzalisha Hewa Tiba (Oxegen Plant) kwenye hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mjini Magharibi iliopo Lumumba ambapo Dola za Kimarekani 104,880 zilitolewa na Mfuko huo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilichangia asilimia 12 ya fedha hizo.

Alisema, kwasasa Zanzibar imefanikiwa kuzalisha Hewa Tiba (Oxegen Plant) kwa hospitali zote za Unguja na Pemba na kuondokana na changamoto hiyo.Aidha, Waziri Mazurui amesema Serikali imefanikiwa kujenga mitambo mikubwa mitatu yakuzalishia hewa hiyo, ambapo mtambo mkubwa unauwezo wa kuzalisha “Oxygen” mita “cube”40 kwa saa iliyounganishwa moja kwa moja na mnyororo wa hewa zilizounganishwa kwenye wodi za kulazia wagonjwa, vyumba vya upasuaji (Theater), chumba cha wagonjwa wenye uangalizi maalum (ICU) na chumba cha dharura (Emergency), hewa hiyo pia imeunganishwa moja kwa moja kutokea kwenye vitanda vya wagonjwa wa vyumba hivyo.

Hata, hivyo Waziri Mazurui amesema ndani ya saa 12 mitambo hiyo hujaza mitungi mikubwa 32 hadi 40 na kusambazwa nchi nzima Unguja na Pemba.