SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesema imepiga hatua kubwa ya kukabiliana na mahitaji ya makazi ya watu wanaoongezeka siku hadi siku, kwa kuzingatia kumudu gharama za nyumba na makaazi endelevu.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo Hotel ya Melia, Kiwengwa, Mkoa wa Kaskazini Unguja, kwenye Mkutano wa mwaka wa pamoja kati Umoja wa Afika na Jumuiya za Taasisi zinazojishughulisha na mikopo ya nyumba kutoka nchi za Umoja wa Afrika (AUHF).

Dk. Mwinyi amezisihi taasisi hizo kutoa mikopo nafuu ili wananchi wamudu kwa gharama nafuu.Ameeleza, Serikali kupitia Shirika la nyumba la Zanzibar (ZHC), imeongeza mipango kadhaa ya kuinua upatikanaji wa nyumba za bei nafuu, hasa kwa familia za kipato cha chini na cha kati ikiwemo ujenzi wa miradi mikubwa ya nyumba iliyoundwa kukidhi mahitaji ya ukuaji wa miji na kuhakikisha Serikali inafanikisha malengo yake.

Rais Dk. Mwinyi pia ameeleza Serikali imeweka kipaumbele cha maendeleo ya jamii endelevu, ikiwemo ujenzi wa nyumba za bei nafuu na kuhakikisha upatikanaji wa huduma muhimu za maji safi, usafi wa mazingira na umeme.Alisema kufanya hivyo ni Kwenda sambamba na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya kujenga maeneo ya mijini iliyopangika.Pia amebainisha kuwa, Serikali inafanya kazi ili kurahisisha michakato ya utowaji ardhi, kuboresha mifumo ya mipango miji na kukuza maendeleo endelevu ya miji ambayo imejengwa ya kudumu.

Amesema, taasisi za kuendeleza Fedha za Afrika ISMMA na Kampuni ya Tanzania Mortgage Refinance Company (TMRC) zinasaidia kuinua maisha ya mamilioni ya Waafrika.Aidha, amesema ushiriki wa AUHF, ISMMA, (TMRC) na wadau wengine hapa Zanzibar unaashiria kuongezeka kwa utambuzi wa kimataifa wa uwezo wa makazi wa Afrika, pia alisema taasisi hizo zinaongeza ushirikiano wa karibu baina ya kujenga mifumo endelevu ya kifedha ya nyumba ambayo itasaidia jitihada za nyumba za bei nafuu sio Afrika pakee bali na duniani kote.

Vilevile Dk. Mwinyi ameielezea Kampuni ya Tanzania Mortgage Refinance Company (TMRC) kwamba ni Mmoja wa washirika wakuu wanaochangia upatikanaji wa fedha za nyumba hasa kwenye kukuza soko la mikopo ya nyumba kwa kutoa fedha za muda mrefu kwa benki na taasisi za fedha, kuziwezesha kutoa bidhaa za mikopo.Halikalika Rais Dk. Mwinyi ameisifu Kampuni ya (TMRC) kwa kuboresha upatikanaji wa mikopo ya nyumba Tanzania, na kuweka wepesi wa umiliki wa nyumba upatikane kwa watu wengi pamoja na kuchochea sekta ya ujenzi, kuzalisha ajira nyingi na kuchangia ukuaji wa uchumi.

Hata hivyo, Rais Dk. Mwinyi amewapongeza wafanyabiashara na taasisi za Kitanzania kwa kupiga hatua na kuendeleza makazi ya gharama nafuu na maendeleo ya mijini wakiwemo Watumishi Housing Company (WHC) ambao ni wahusika waku katika kushughulikia mahitaji ya makazi ya Watanzania, Benki Kuu ya Tanzania na CRDB inayoongoza kwa utoaji wa ufadhili wa mikopo ya nyumba kwa wananchi.

Akizungumza kwenye Mkutano huo Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar, Rahma Kassim Ali amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza ushirikiano wake na taasisi hizo za nyumba hasa katika kuwajengea wananchi nyumba zenye ubora na kwa harama nafuu.