MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapindizi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya uwekezaji na shughuli za biashara ili kukuza uchumi na kuongeza fursa nyingi za ajira kwa vijana.Amesema tayari Serikali imesajili na kutenga zaidi ya miradi 330 yenye thamani ya mtaji wa USD bilioni 5.4 ili kuzalisha ajira zaidi ya 18,000 kwa sekta mbalimbali zikiwemo, utalii yenye miradi 112, biashara ya majengo 56, viwanda 36 na sekta nyengine.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo viwanja vya Gombani Mkoa wa Kaskazini, alipozindua Kampeni ya Kijana Kijani Pemba ikiwa ni shamrashamra za kupongeza miaka minne ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nane, anayoiongoza.Dk. Mwinyi amesema, Serikali imetoa vifaa vya uzalishaji kwa vijana vyenye thamani ya TZS 985,503,931 kwa vikundi 420 pamoja na ruzuku ya TZS 338,611,431 kwa vikundi 395 vya vijana ili kuwainua na kuwawesha kiuchumi.
Katika kuhakikisha wananchi wanapata mitaji ya kuendesha shughuli zao, Rais Dk. Mwinyi amebainisha kuwa, Serikali hadi kufikia mwezi Machi, 2024 kupitia Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi tayari imetoa zaidi ya TZS Bilioni 31.8 kwa wajasiliamali wadogo wadogo Unguja na Pemba, ambapo asilimia 40 ya wanufaika ni vijana wa umri kati ya miaka 18- 35.
Aidha, ameeleza kujengwa kwa vituo vya wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo kwa kila Wilaya ni kuwawezesha wananchi wa Zanzibar kwa kuwapa maeneo mazuri ya kufanya shughuli zao na kuzalisha fursa za ajira.Akizungumzia nia ya Serikali kuendeleza juhudi ya kuifungua Pemba kimaendeleo Rais Dk. Mwinyi amesema Serikali imeendeleza kazi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara kuu na za vijijini, kutengeneza bandari za Mkoani na Shumba na kuanza matayarisho ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Pemba.
Pia Dk. Mwinyi amebainisha kuwa Serikali inaendelea kuimarisha eneo la uwekezaji la Micheweni na eneo la viwanda Chamanangwe kwa kuyawekea miundombinu nakuongeza kuwa, tayari kuna wawekezaji waliojitokeza kuwekeza maeneo hayo hatua aliyoieleza kwamba itaongeza fursa za ajira kwa vijana.Akizungmzia juu ya kuimarisha shughuli za biashara na ujasiriamali kwa vijana Rais Dk. Mwinyi ameeleza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya nane ya ujenzi wa masoko makubwa ya kisasa likiwemo Mwanakwerekwe, Jumbi na Chuini ambayo mawili tayari yashafunguliwa.
Akizungumza kwenye hadhara hiyo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amewazungumzia wananchi wa Pemba kwamba wanafahamu thamani ya maendeleo na kuona juhudi za Rais Dk. Mwinyi pia amewaelezea Wazanzibari kwa ujumla wao kuwa wanaupenda uongozi wa Serikali yote ya Awamu ya nne sambamba na kuwasihi wananchi wa Zanzibar kujihusisha na siasa ni Maendeleo sio ugomvi.
Naye, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi, UVCCM na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Ndg. Joketi Mwegelo, amesema CCM itashinda kwa ushawishi na imani kubwa kwa viongozi wao na kubainisha kuwa Chama hicho hakiyumbishwi kwa chokochoko na majungu ya uvunjifu wa amani bali misimamo ya viongozi wa kuu wa Nchi wanaohubiri na kusisitiza umoja, utulivu, msikamamo na uthubutu.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mattar Zahor Masoud akiwawakilisha wananchi wa Mikoa miwili ya Pemba Kusini na Kaskazini amepongeza juhudi kubwa ya maendeleo iliyofanywa ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dk. Mwinyi na kusifu hatua ya Serikiali ya Mapinduzi ya Zanzibar kujenga madarasa 661kwa Mikoa yote ya Pemba skuli za ghorofa 13, ajira za walimu 1500 kutolewa vibali vya ajira za walimu, 600 ujenzi wa vyoo 953 kwa skuli mbalimbali, ujenzi wa hospitali kwa Wilaya tatu za Pemba, ujkarabati mkubwa kwa hospitali ya Abdalla Mzee, kuongezwa kwa chumba cha ICU na Dialysis na ajira za 468 Sekta ya Afya na huduma nyengine za jamii.
Kampeni ya “Kijana Kijani” yenye kauli mbiu “Tunazima zote tunawasha kijani” imefanikiwa kuingiza wananchama wapya 1135 kutoka chama cha upinzani cha ACT Wazalendo, wakiwemo wanachama mashuhuri na viongozi waandamini wa chama hicho.