Akitoa salamu zake za mwaka mpya wa 2014 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amebainisha kuwa Zanzibar ikiyafikia malengo yake maendeleo sio tu kutachochea ari na hamasa kwa wananchi wake bali hata kwa washirika wake wa maendeleo na Jumuiya ya Kimataifa.Kwa hiyo amewakumbusha wananchi wajibu wao wa kuitumika nchi pamoja na kuimarisha na kuendeleza umoja na ushirikiano, amani, utulivu na mapenzi baina yao.
Katika mnasaba huo ametoa wito kwa wananchi kuacha kufanyakazi kwa mazoea na kwa watumishi wa umma wafanye kazi kwa kutimiza wajibu wao kwa kuzingatia Sheria ya Utumushi wa Umma na Kanuni zake
Dk. Shein amesema amefurahishwa sana kuona katika kipindi hiki Zanzibar inaadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi wananchi wamekuwa wakionesha mshikamano, upendo na uzalendo bila kujali itikadi zao za kisiasa na ubaguzi.Hali hiyo ameielezea kuwa ni uthibitisho wa kutosha wa mapenzi baina ya wananchi na kwa nchi yao.
Kwa hiyo ametaka wananchi wazidi kuzingatia kuwa wana wajibu wa kuendelea kuyatetea, kuyalinda, kuyaenzi na kuyaendeleza Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964.Katika salamu hizo Dk. Shein amewataka wananchi wajiandae pia kwa maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano yatakayofanyika mwezi April mwakani na kusisitiza kuwa Muungano huo ndio msingi wa kuimarisha udugu wa wananchi wa Zanzibar na Tanzania Bara.
Ametoa wito kwa wananchi kushiriki katika maonyesho ya Miaka 50 ya Mapinduzi ambayo anatarajia kuyazindua rasmi tarehe 2 Janauri, 2013.