BISMILLAHI RAHMAN RAHIM
Naanza kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na Mwenye kuneemesha neema zote ndogo ndogo.
Ndugu Wananchi,
Assalamu Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuhu.
Ni wajibu wetu kumshukuru Mola wetu (SW) kwa kutujaalia neema ya uhai na leo hii tukajaaliwa kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu aliyelijaaliya jua kuwa na mwangaza, na mwezi ukawa na nuru, na akaupimia vituo ili tujue idadi ya miaka na hisabu yake. Tunamuomba atujaaliye siha, nguvu na uwezo kwa kuitekeleza ibada ya Saumu katika mwaka huu 1437 Hijria, kwa unyenyekevu, utiifu na katika hali ya amani na utulivu.
Tunamshukuru Mola wetu kwa kutuwezesha kujuumuika na waislamu wenzetu katika nchi mbali mbali leo hii katika kuukaribisha mwezi huu mtukufu. Ni neema na hidaya kubwa kwetu tukizingatia kuwa wako wenzetu tuliofunga nao Ramadhani iliyopita, na leo hii hatunao tena, wametangulia mbele ya haki. Tunamuomba Mwenyezi Mungu uwasamehe makosa yao na awape makaazi mema Peponi wale wote waliotangulia mbele ya haki. Amin.
Ndugu Wananchi,
Wakati tunaukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, ni vyema tukakumbushana baadhi ya mambo muhimu yanayopendeza kufanywa katika mwezi huu.
Huu ni Mwezi Mtukufu ambao ndani yake imeteremshwa Qur’ani kama alivyotubainishia Subahana Wataala katika Kitabu chake kitukufu cha Qur’ani katika aya ya 185 ya Suratul Baqara, kwa kusema:
“Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa ndani yake Qur-an kuwa ni uongofu kwa watu, na hoja zilizowazi za uwongofu na upambanuzi .. …………” (2:185)
Ilivyokuwa katika mwezi huu ndio Qur’ani iliteremshwa kwa Mtume wetu Muhammad (SAW), tuna wajibu wa kufanya bidii katika kuisoma na kuifahamu Qur’an, ili tuweze kuishi kama Mwenyezi Mungu alivyotuelekeza na tupate baraka zake hapa duniani na kesho mbele ya haki.
Vile vile, hatuna budi kuhimizana katika kuzitekeleza Sala za Fardhi na kusali Sala za Sunna mbali mbali hasa katika nyakati za usiku. Huu ni mwezi, ambao ndani yake unapatikana usiku wenye heshima kubwa (Laylatul Qadr) ambao ibada ya usiku huo imebarikiwa kuliko ibada ya miezi elfu moja, na kwa hekima yake, Allah (SW), hakutubainishia kuwa ni usiku wa tarehe ngapi.
Bwana Mtume Muhammad (SAW) amesema:
“Mwenye kusimama usiku wa Ramadhani kwa kufanya ibada hali ya kuwa na imani na kutaraji thawabu, anasamehewa mtu huyo, yote yaliyotangulia miongoni mwa makosa yake.”
(Bukhari na Muslim).
Ndugu Wananchi,
Vile vile, ni muhimu katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani tukakumbushana kuwa miongoni mwa ibada tukufu alizokuwa akizifanya Bwana Mtume (SAW) ni kutoa sadaka na alilipa umuhimu sana jambo hili hadi wakati wa kuondoka kwake duniani. Wakati Bwana Mtume Muhammad (S.A.W) alipokuwa katika sakaratul mauti kila alipopata fahamu alikuwa akimuuliza Bibi Aisha (‘Radhiyallahu Unha) iwapo ameshazitoa sadaka zile dirhamu nne zilizokuwa nyumbani kwake wakati huo. Kadhalika, kutoa kwake sadaka kulikuwa kukiongezeka katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Ni wajibu wetu tuishi, yeye akiwa ni mfano wa umma huu.
Vile vile, tufanye bidii na kumtaja Allah, tufanye istighfari na kukaa Itikafu, tuharakishe kufungua wakati unapofika na tutekeleze sunna ya kula daku. Mambo haya yote yamepewa uzito mkubwa katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Tumuombe Allah atupe nguvu na uwezo wa kuyatekeleza mambo haya.
Ndugu Wananchi,
Sambamba na kuongeza juhudi katika kufanya mambo mema, ni wajibu wetu tuongeze juhudi katika kujizuwia ili tusifanye mambo maovu yaliyokatazwa ambayo yanaweza kubatilisha funga zetu au kufanya mambo ambayo hayapendezi kufanywa na mtu aliyefunga na yanayoweza kupunguza uzito wa mizani ya thawabu katika ibada zetu.
Wakati tunajiandaa na kufunga, ni muhimu sote tukafahamu kwamba hivi sasa teknolojia imevisongeza vishawishi vingi vinavyoweza kuibatilisha saumu karibu na nafsi zetu. Miongoni mwa vishawishi hivyo ni mitandao ya simu na intaneti.
Nimeona nikukumbusheni ndugu wananchi, kuhusu suala hili, kwa sababu nahisi bado tunachangamoto mbali mbali za kijamii na kidini zinazoibuka kutokana na matumizi mabaya ya mitandao. Bila ya kujijua, mtu anaweza kujikuta anafanya makosa pale anapoangalia mitandao yenye mambo yasiyopendeza, hasa katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Simu zimerahisisha mawasiliano katika jamii yetu, lakini vijana wetu wa kike na wa kiume, hufanya mazungumzo ya faragha yasiyoruhusiwa kidini baina ya vijana hao. Ni wajibu wetu waislamu tujiepushe na vitendo vinavyoweza kubatilisha saumu zetu kwa njia ya mitandao ya simu na kompyuta.
Wito wangu kwa mashekhe ni kwamba waendelee kutoa taaluma juu ya umuhimu wa matumizi bora ya mitandao na kwa pamoja tuhimizane juu ya umuhimu wa kuunga mkono juhudi zetu zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali za kushajihisha matumizi bora ya mitandao ya simu na kompyuta kwa kutumia mitandao ya intaneti.
Ndugu Wananchi,
Ni muhimu tukazingatia kuwa wakati tunaukaribisha Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani bado tumekabiliwa na tatizo la kuwepo kwa miripuko ya maradhi ya kipindupindu katika sehemu mbali mbali za Unguja na Pemba. Hadi leo ambapo tunaukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani bado wapo wagonjwa wanaohudumiwa katika vituo vinavyotolewa utibabu wa maradhi ya kipundupindu, Unguja na Pemba.
Hali ya maradhi hayo yalipofikia hivi sasa ni nafuu sana, ikilinganishwa na kipindi cha wiki iliyoanzia tarehe 16 hadi 22 Aprili, 2016 ambapo wagonjwa wa kipindupindu walifikia 250 kwa Unguja na Pemba ndani ya wiki moja. Tunapaswa tuyadhibiti maradhi hayo kwa juhudi zetu zote.
Ndugu Wananchi,
Katika kuendeleza jitihada na mikakati ya kuyanusuru maisha ya wananchi na kujikinga na miripuko ya kasi ambayo inaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa harakati za maisha yetu na mwenendo mzima wa uchumi, Serikali itaendelea kuchukua tahadhari kwa kuchukua hatua mbali mbali kama zilivyotangazwa na Wizara ya Afya.
Serikali inajuwa kwamba uamuzi huu uliochukuliwa unaweza kuathiri utamaduni wetu wa kuandaa hafla na tafrija za kufutarisha zinazoandaliwa na wananchi, taasisi mbali mbali za Serikali na sekta binafsi katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Imani yangu ni kuwa, sote tutaendelea kushirikiana katika kuendelea kulitekeleza agizo hilo la Serikali, lengo letu liwe ni kushirikiana katika kuyanusuru maisha yetu kwa kuyatokomeza maradhi haya kwa haraka zaidi ili tuweze kuendesha shughuli na harakati za maisha katika hali ya kawaida.
Nasaha zangu kwenu wananchi ni kuwa tuendelee kufuata miongozo ya usafi iliyotolewa na wataalamu wa afya na Serikali inaendelea kufanya tathmini kuhusu hali hiyo na itawapa taarifa kwa kadri hali inavyoendelea kuimarika.
Ndugu Wananchi,
Ni muhimu tukakumbushana kuwa Bwana Mtume Muhammad (S.AW) alikuwa akizidisha ukarimu katika mwezi huu wa Ramadhani. Siku zote alikuwa mkarimu, lakini alikuwa mkarimu zaidi katika mwezi huo. Kwa hivyo, ni wajibu wetu kufuata nyendo za Kiongozi wetu kwa kuzidisha ukarimu baina yetu katika Mwezi Mtukufu tunaouanza kesho.
Inasikitisha kuona kuwa, licha ya kuwa uislamu unahimiza kuoneana huruma, lakini wapo wafanyabiashara ambao huchukua fursa ya kupandisha bei bidhaa zao katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan, hasa zile bidhaa za chakula muhimu ambazo Serikali hupunguza ushuru ili kuwapa afueni wananchi. Nafahamu malalamiko yaliyopo hivi sasa, ambapo wafanyabiashara walipandisha bei za bidhaa kwa kisingizio cha uchaguzi. Hadi leo hii bei za bidhaa hizo bado ziko juu.
Serikali itaongeza juhudi za kuwafuatilia wafanyabiashara wenye tabia hiyo ya kupandisha bei za bidhaa muhimu bila ya sababu za msingi, jambo ambalo linaathiri hatua ya Serikali ya Mapinduzi ya kutoa unafuu wa ushuru wa bidhaa muhimu kwa wafanyabiashara, ili waziuze bidhaa hizo kwa wananchi kwa bei nafuu. Kadhalika, upandishaji wa bei usio na msingi unakwenda kinyume na malengo yetu ya kuanzishwa kwa biashara huru yenye ushindani. Serikali itaendelea kushirikiana na wafanyabiashara na itahakikisha kuwa bidhaa zote muhimu zinazohitajika na kutumika zaidi katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani zinapatikana wakati wote na bila ya usumbufu wowote.
Ndugu Wananchi,
Miongoni mwa mambo muhimu kwa waislamu ni kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwetu. Mtume Muhammad (S.A.W) katika maisha yake amehimiza sana suala la kuvumiliana, kupendana na kustahamiliana na kuishi bila ya kukhitilafiana kwa mambo madogo madogo.
Kadhalika, Mtume Muhammad (SAW) ametufundisha umuhimu wa kudumisha umoja na udugu kwa kutwambia:
“Msikate ujamaa, msigeuke, msichukiane na msihusudiane. Nyinyi mkiwa ni waja wa Mwenyezi Mungu, dumisheni udugu. Ndugu wawili wasinuniane kwa zaidi ya siku tatu” (Imepokewa na Imam Malik).
Katika hadithi nyengine Mtume Muhammad (S.A.W) anatufundisha kwamba:
“Tabasamu unayoonesha kwa nduguyo ni sadaka” (Tirmidh).
Qur-ani Tukufu, inahimiza suala la kukuza udugu kwa kutwambia katika aya ya 10 ya Surat al-Hujurat
“Kwa hakika Waislamu wote ni ndugu basi patanisheni baina ya ndugu zenu na mcheni Mwenyezi Mungu ...” (49:10).
Kutokana na mafundisho hayo ya Qur’ani na Hadithi za Mtume wetu Muhammad (S.A.W) ni wajibu wetu wa kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa anafanya vitendo vyema, anaepuka chuki na hasama na kuimarisha mapenzi miongoni mwa Wazanzibari wote.
Tuimarishe mshikamano wetu katika kulinda amani ili tuweze kuitekeleza saumu na ibada nyengine katika hali ya amani na utulivu, tukitambua kuwa amani ndio msingi unaotuwezesha na kutupa uhuru wa kufanya ibada kwa utulivu na kutafuta riziki za halali kwa familia zetu.
Ni wajibu wetu kumshukuru Mwenyezi Mungu Muweza kwa kuiweka nchi yetu katika hali ya amani na salama na sote tunafahamu kuwa sisi ni wamoja na kwa hivyo, chuki na husda hazina tija wala hazina nafasi katika kuijenga Zanzibar ya leo.
Napenda nikuhakikishieni ndugu wananchi kuwa, Serikali zetu mbili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya amani na salama.
Ndugu Wananchi,
Nafahamu kwamba licha ya jitihada mbali mbali zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kuwapatia wananchi huduma bora za jamii, lakini bado huduma hizo hazipatikani vizuri katika baadhi ya maeneo. Kwa mfano, bado shida ya maji safi na salama inaendelea kuwakumba wananchi katika baadhi ya maeneo.
Kwa hivyo, katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, bado wananchi wanaoishi katika maeneo hayo wanaweza kupata shida ya ukosefu wa maji. Kutokana na hali hiyo, kwa mara nyengine ninaiagiza Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira pamoja na Mamlaka ya Maji ya Zanzibar (ZAWA) ifanye kila jitihada ili iwapatie wananchi maji safi na salama, kwa kutumia magari katika sehemu zote ambazo zina upungufu wa maji safi na salama. Mkurugenzi Mkuu wa ZAWA ahakikishe kwamba kazi hii ya kuwapatia wananchi maji inafanyika kwa mafanikio makubwa. Natoa wito kwa wananchi washirikiane na Mamlaka hiyo ili waifanikishe shughuli hiyo ipasavyo.
Ndugu Wananchi,
Napenda nimalizie risala yangu kwa kukutakieni nyote kheri, rehema na baraka za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Namuomba Mwenyezi Mungu atuzidishe mapenzi baina yetu na aizidishe baraka na neema katika nchi yetu.
Ramadhani Njema.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.