RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya kilimo na kuwapongeza Washirika wa Maendeleo wa sekta hiyo waliopo nchini kwa kuiunga mkono dhamira hiyo.
Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo alipokutana na kufanya mazungumzo na Washirika wa Maedeleo wa Sekta ya Kilimo Tanzania wakiongozwa na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Chakula na Kilimo Dudiani (FAO) ambaye pia, ni Mwenyekiti wa Washirika hao hapa nchini Fred Kafeero.
Katika Mazungumzo hayo, Dk. Shein alipongeza hatua kubwa zilizochukuliwa na Washirika hao wa Maendeleo wa sekta ya Kilimo kwa kufika Zanzibar na kuja kuona juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika sekta hiyo na hatimae kupata upeo mpana wa kupata kujua mafanikio na changamoto zilizopo.
Rais Dk. Shein alieleza matumaini yake kutokana na azma na mikakati iliyowekwa na Washirika hao wa Maendeleo katika kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya kilimo hasa katika programu kuu ya Sekta ya Kilimo hapa Zanzibar ambayo ipo katika hatua ya mwisho ya matayarisho.
Alieleza kuwa hatua za Washirika hao wa Maendeleo ya kuja Zanzibar kwa muda wa siku mbili kwa lengo na azma ya kutembelea maeneo mbali mbali ya sekta ya Kilimo pamoja na kuwepo rasimu ya programu ya sekta ya kilimo ili kuona maeneo ambayo watashirikiana ni jambo jema na linatoa mwanga wa matumaini katika sekta hiyo.
Aidha, Rais Dk. Shein alisisitiza haja kwa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kuhakikisha Programu Kuu ya Sekta ya Kilimo Zanzibar ambayo itakuwa ndio Dira katika mashirikiano ambayo Zanzibar itaonesha mipango ya sekta ya kilimo kwa hivi sasa na miaka mengine ijayo.
Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein aliwapongeza Washirika wote wa Maendeleo wa sekta ya Kilimo Tanzania na kulipongeza Shirika la (FAO), kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya kilimo na kuifanya izidi kuvutia kwa kutoa ajira kwa vijana sambamba na kuimarisha uchumi wa nchi.
Rais Dk. Shein pia, alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Jumuiya ya Ulaya (EU), kwa kuendelea kushirikiana na Zanzibar katika kuendeleza miradi mbali mbali ya maendeleo hasa katika kufanya utafiti wa kutafuta nishati mbada.
Alieleza kuvutiwa kwake na juhudi zinazochukuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Viwanda Duniani (UNIDO) kwa kuendeleza viwanda vidogo vidogo hapa Zanzibar kwa lengo la kusaidia sekta ya ajira sambamba na matumizi bora ya bidhaa za kilimo.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alieleza haja kwa Shirika la Maendeleo ya Kilimo la Umoja wa Mataifa (IFAD) kuhakikisha linaendelea kufanya kazi kwa karibu zaidi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili Zanzibar iweze kunufaika na miradi inayoendeshwa na Shirika hilo.
Nao Washirika hao wa Maendeleo wa Sekta ya Kilimo Tanzania wakiongozwa na Mwenyekiti wao Fred Kafeero ambaye pia ni Mwakilishi wa (FAO) nchini Tanzania walimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuiendeleza sekta ya kilimo na kuiunganisha na sekta nyengine ili ziweze kwenda sambamba na mipango ya maendeleo iliyopangwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Walieleza kwamba kasi ya uchumi inaimarika zaidi pale sekta zote muhimu za kiuchumi na kujamii zinapofanya kazi kwa kasi ya pamoja kama alivyoamua kufanya hivyo Rais Dk. Shein katika sekta hiyo ya kilimo.
Aidha, viongozi hao walieleza kufurahishwa kwao kwa kupata fursa ya kuitembelea Zanzibar na kujua mafanikio na changamoto zilizopo katika sekta ya kilimo na kuahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar.
Viongozi hao waliahidi kutoa ushirikiano wao katika uhamasishaji na ushahijishaji katika kutafuta rasilimali muhimu zinazohitajika katika kuendeleza sekta ya kilimo hapa Zanzibar sambamba na kuhakikisha programu kuu ya Sekta ya Kilimo Zanzibar inafanikiwa.
Sambamba na hayo, walieleza haja kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuzichangamkia na kuzitumia vyema fursa zilizopo kutoka kwa Wasirika wa Maendeleo wa Sekta ya Kilimo Tanzania hasa katika suala zima la upatikanaji wa misaada na mikopo.
Walieleza kuwa nchi nyingi wameweza kupata mafanikio na kuendeleza sekta ya kilimo kwa kuzitumia vizuri fursa za mikopo na misaada inayotolewa huku kiongozi wa Umoja wa Ulaya aliyekuwemo katika ujumbe huo Bi Jenny Correian Nunes akiahidi Jumuiya hiyo kuendelea kutoa ushirikiano wake kwa Zanzibar.
Viongozi hao walieleza kuvutiwa kwao na kauli ya Rais Dk. Shein anayoitoa mara kwa mara juu ya utendaji wa kazi kwa kuwataka watendaji kwenda kwenye maeneo ya kazi badala ya kukaa maofisini kauli ambayo walieleza kuwa ndio Dira kubwa katika utekelezaji wao wa kazi.