RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amewaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni kushika nyadhifa mbali mbali katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Viongozi walioapishwa ni Salum Kassim Ali aliyeapishwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambapo kabla ya uteuzi wake alikuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi katika Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).
Wengine ni Asma Hamid Jidawi aliyeapishwa kuwa Katibu wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma Zanzibar na Thabit Idarous Faina aliyeapishwa kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi katika Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).
Mara baada ya kuapishwa viongozi hao kwa nyakati tofauti walieleza jinsi walivyopokea uteuzi wao huo na kutoa pongezi zao kwa Rais Dk. Shein kwa kuwateua na kuwaamini kuwa wanaweza kufanya kazi walizopewa katika nafasi walizoteuliwa.
Viongozi hao waliahidi kuitumikia, kuilinda Zanzibar pamoja na watu wake kwa kufuata misingi ya Sheria, taratibu na miongozo ya nchi na kuahidi kutoa mashirikiano kwa viongozi na watendaji wote huku wakieleza matumaini yao na wao kupata mashirikiano hayo.
Hafla hiyo, ilifanyika Ikulu mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Said Hassan Said, Mawaziri na Manaibu Mawaziri.
Wengine waliohudhuria katika hafla hiyo ni Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud, Washauri wa Rais wa Zanzibar pamoja na viongozi wengine wa Serikali.