Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa kufanya mashindano ya kuhifadhi na kusoma Qur’an katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ni fursa nyengine ya ibada na fadhila za kusoma Qur’an ndani ya mwezi huu.Alhaj Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo Masjid Zenjbar Mazizini katika fainali ya Mashindano ya Kimataifa ya kuhifadhi Qur’an yaliyozishirikisha nchi mbali mbali katika Bara la Afrika.
Katika hotuba yake, Alhaj Dk. Mwinyi alieleza kwamba Uislamu unahimiza katika mwezi huu wa Ramadhani kufanyike jitihada katika kukithirisha kusoma sana Qur’an kwani huu ndiyo mwezi iliyoteremshwa katika usiku wa Laylatul Kadr.Aliongeza kuwa utaratibu huu wa mashindano ya kuhifadhi na kusoma Qur’an ni kuwaandaa Maulamaa na Masheikh wa baadae.
“Hili ni jambo jema linalojenga misingi mizuri ya Dini kwa vijana tangu wangali na umri mdogo na kuwafanya wakue wakiwa wameandaliwa vyema katika maisha ya ucha mungu na kufanya mambo ya kheri”,alisema Alhaj Dk. Mwinyi.Aidha, aliipongeza kwa dhati na kuishukuru sana Jumuiya ya Kuhifadhisha Qur’an Zanzibar kwa kuwa mstari wa mbele katika kuliendeleza jambo hilo la kheir tokea kuanzishwa kwa Jumuiya hii miaka 30 iliyopita.
Alitoa shukurani kwa Waislamu na wafadhili wote wanaohamasika kuchangia kwa namna moja au nyengine katika kuhakikisha mashindano ya kuhifadhi na kusoma Qur’an yanafanyika na kupata mafanikio kila mwaka.Aliwapongeza wazazi kwa kuona umuhimu wa kuwasaidia vijana kushiriki katika mambo kama hayo ya kheri na kutoa shukurani maalum kwa walimu na Masheikh waliowaandaa kwa kuwasomesha vijana washiriki hadi wakaweza kufikia hatua hiyo ya fainali ya mashindano ya mwaka huu.
Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Mwinyi alitoa wito kwa Waislamu wote kujenga utamaduni wa kuchangia masuala mbali mbali yenye mnasaba wa kuimarisha Uislamu ikiwemo kusaidia ujenzi wa madrsa, misikiti pamoja na vituo vya Kiislamu.
Alhaj Dk. Mwinyi pia, alipokea ombi la Jumuiya hiyo la kuwasaidia vijana waliohifadhi Juzuu 30 za Qur’an waliomaliza kidato cha Sita ambao wana sifa za kuendelea katika masomo ya chuo kikuu ambao hawakupata ufadhili wa masomo yao atawaunga mkono kwa kuwasaidia kuwatafutia wadhamini.Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Mwinyi aliahidi kuiunga mkono Jumuiya hiyo katika ujenzi wa kituo chao cha mafunzo ya kuhifadhi Qur’an kinachotarajiwa kujengwa na Jumuiya hiyo.
Nae Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi alieleza umuhimu wa kuhifadhi Qur’an na kueleza imani aliyokuwa nayo kwa vijana hao ya kuuendeleza Uislamu katika nchi zao mbali mbali wanazotoka.Mapema Amiri wa Jumuiya hiyo Sheikh Suleiman Omar Ahmed alitoa pongezi kwa Alhaj Dk. Mwinyi kwa kuungana nao katika mashindano hayo na kueleza uzoefu wa Jumuiya yao ambayo imetimiza miaka 30 tokea kuanzishwa kwake.
Alieleza kuwa matunda ya Jumuiya hiyo yanaonekana hivi sasa ambapo imepelekea kuzalisha vijana wengi waliohifadhi Qur’an pamoja na nchi nyingi katika Bara la Afrika kujitokeza kuja kushiriki katika mashindano hayo.Pia, Sheikh Suleiman alitumia fursa hiyo kuwaombea vijana waliohifadhi Juzuu 30 za Qur’an waliomaliza kidato cha sita na wana sifa za kuendelea chuo kikuu kuwatafutia ufadhili ili wapate kujiendeleza katika elimu ya dini na dunia.
Katika mashindano hayo ya Juzuu 30 Hifdhi yaliwashirikisha wanafunzi 13 kutoka Zanzibar, Tanzania Bara, Kenya, Rwanda, Uganda, Burundi, Malawi, Niger, Msumbiji, Comoro, Nigeria na Chad.
Alhaj Dk. Mwinyi alitoa zawadi kwa washindi na washiriki wote ambapo mshindi wa kwanza katika mashindano hayo alikuwa Hissein Youssouf Adam kutoka Chad na wa pili ni Saidi Doushimana kutoka Rwanda na mshindi wa tatu ni Hassane Djibrilla Oumarou kutoka Niger na wa nne ni Muslim Salum Seif kutoka Zanzibar.
Sambamba na hayo, mashindano mengine ya Juzuu 30 yalikuwa ni Tashjee Tahqiq yaliyowashirikisha washiriki wanne ambapo mshindi wa mwanzo alikuwa ni Nassir Rashid Seif kutoka Zanzibar na mshindi wa pili ni Rashid Hemed Rashid kutoka Zanzibar na wa tatu ni Mbarouk Mussa Juma kutoka Zanzibar na mshindi wa nne alikuwa ni Ahmad Kongo Kaginya kutoka Kenya