Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema kwa kipindi cha miaka mingi, China imekuwa mshirika muhimu katika ukuaji wa uchumi Zanzibar kupitia uwekezaji na sekta mbalimbali hususan miradi ya ujenzi wa miundombinu. China ina jumla ya miradi 17 ya uwekezaji iliyosajiliwa Zanzibar yenye thamani ya takriban dola za Kimarekani milioni 245, ambayo imetoa ajira za moja kwa moja kwa wananchi wa Zanzibar zipatazo 8,000.
Aidha, China ni mshirika wa pili kwa ukubwa katika uagizaji wa bidhaa kutoka Zanzibar, ambapo thamani ya biashara baina ya nchi hizo mbili imepanda kwa kasi kufikia dola milioni 66.5 mwaka 2023. Ushirikiano huu umetoa mchango mkubwa kwa kukuza sekta za kilimo, viwanda, na biashara.
Rais. Dk. Mwinyi ameyasema hayo katika Warsha maalum ya kukuza Uwekezaji, Biashara na Utalii iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Waldorf Astoria jijini Shanghai, iliyoandaliwa na Mamlaka ya Kukuza Uwekazaji Zanzibar (ZIPA) kushirikiana na Ubalozi wa China, Tanzania.
Warsha hiyo ni hatua muhimu ambayo itaimarisha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya Zanzibar na China, ikilenga kuendeleza ushirikiano wa uwekezaji pamoja na kuongeza fursa za biashara, teknolojia na kubadilishana ujuzi.
Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi ameshuhudia utiaji saini wa mikataba mbalimbali ya kibiashara inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na China. Miongoni mwa mikataba hiyo ni pamoja na Zanzibar Seaweed Company kutoka Zanzibar na Dafeng Huixiang Biochemical Products Company kutoka China, Shandong Export & Credit Insurance Corporation na Weihai Huatan Supply Chain Management Co. Ltd, Sisalana Tanzania Company Ltd na Shanghai Linghang Group. Mikataba hiyo inalenga kuimarisha biashara, ikijumuisha teknolojia ya kisasa ya masoko ya kimataifa, usimamizi wa bidhaa kwa mujibu wa viwango vya kimataifa, kuongeza thamani ya bidhaa na kutoa ajira kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini China, Mhe. Khamis Mussa Omar, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) Saleh Saad Mohamed, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) Juma Burhan, Bi. Latifa M Hamis Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) na viongozi mbalimbali wa Serikali Tanzania na China, Wawekezaji na Wafanyabiashara.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, amemaliza ziara yake ya kikazi nchini China, ambapo alihudhuria ufunguzi wa Maonesho ya 7 ya China International Import Expo (CIIE) na kutembelea mabanda ya washiriki mbalimbali wa maonesho hayo. Katika ziara hiyo, Rais Mwinyi alikutana na viongozi waandamizi wa Serikali ya China, viongozi wa makampuni mbalimbali, na wawekezaji, ambapo walijadiliana kwa kina masuala ya kibiashara, uwekezaji, na mipango ya maendeleo endelevu kwa manufaa ya pande zote mbili.