MKE wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Mama Mariam Mwinyi ameipongeza na kuishukuru taasisi ya “Merck Foundation” kwa uamuzi wao wakuichagua Tanzania kuweka Mkutano wao wa 11 ambao umedhihirisha wazi ushirikiano baina ya Afrika na taasisi hiyo.
Mama Mariam Mwinyi ambae pia ni Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation” (ZMBF), ametoa pongezi hizo kwenye Mkutano wa 11 wa “Merck Foundation Africa Asia Luminary”, uliowakutanisha pamoja wake wa Marais wa Afrika kutoka nchi 15, huko hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam.
Mama Mariam, ameeleza kufurahishwa kwake na mchango mkubwa wanaoutoa wake wa Marais wa Afrika hasa katika kutoa ufadhili wa Masomo kwa fursa 2080 kwa madaktari chipukizi kwa nchi 52 za Afrika kwa taaluma muhimu 44 zenye uhitaji zikiwemo ‘oncology”, utaalamu wa afya ya uzazi kwa kina mama, maradhi ya kisukari na maradhi mengine.
Akizungumzia masuala ya unyanyapaa na udhalilishaji kwa kinamama, wasichana na watoto, Mama Mariam Mwinyi amepongeza ushirikiano wa pamoja kwa wake wa viongozi wakuu wa Afrika kwa umoja wao kushughulikia masuala ya kikatili kwa wanawake na jamii ya Afrika ikiwemo kuvunja unyanyapaa hasa wa wanawake wagumba ambao wamekua kikwazo kikubwa kwa baadhi ya jamii za Afrika.
Pia, Mama Mariam Mwinyi amewapongeza wanawake wa viongozi hao kwa kusaidia jamii zao masuala ya elimu kwa wasichana, kukomesha ndoa za utotoni na ukeketaji (FGM), kupinga ukatili wa kijinsia, na kuwawezesha kiuchumi wanawake na wajane.
Katika hatua nyengine, Mama Mariam Mwinyi ameeleza shauku yake ya kuendelea kushirikiana na wanawake wenziwe wake wa viongozi wakuu wa bara la Afrika kutokana na maendeleo na hatua kubwa walizopiga mataifa mengine ya Afrika.
Ametumia fursa hiyo kuipongeza “Merck Foundation” kwa kutimiza miaka 12 ya utekelezaji wa miradi yake ya maendeleo kwa nchi za Afrika na Asia pamoja kutimiza miaka saba tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo.
Aidha, ameeleza mafanikio hayo yanaimarisha kujitolea kwa “Merck Foundation” kwenye kuendeleza utunzaji wa mazingira hasa kwa wagonjwa sambamba na kuwainua kimaendeleo, kuwajengea uwezo wananwake na wasichana wa Afrika kwa kuwaongezea viwango vya taaluma.
Akishirikisha uzoefu wa taasisi yake ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation” (ZMBF) kwenye Mkutano huo, Mama Mariam Mwinyi ameeleza dhamira ya taasisi hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2021, ni kujitolea zaidi kuimarisha ustawi wa jamii, kuboreha maisha bora kwa wote lengo ikiwa ni kuboresha lishe na huduma bora za afya ya uzazi, watoto wachanga, watoto na vijana.
Akizungumzia kampeni za “Afya Bora, Maisha Bora”, na ya “Mariam Mwinyi Walkathon” alieleza kwamba zimelenga kushajihisha jamii juu ya maisha na ustawi wa afya ambapo kampeni hizo zilifanikiwa kuifikia jamii ya Zanzibar.
Mama Mariam Mwinyi amesema ZMBF imefanikiwa pia kuwafikia wanajamii 17,000 kwa huduma za afya ya uzazi, huduma ya mama na mtoto pamoja na kushughulikia magonjwa yasiyoambukiza.
Ameeleza ZMBF kupitia mradi wake wa “Tumaini Kits” unaolenga afya ya uzazi, umefikia wasichana 5,033 walioko shuleni, na kuwapatia taulo za kike, kwajili ya hedhi salama.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Wenyemahitaji Maaluu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Dorothy Gwajima amesema, mkutano huo haukujadili masuala ya afya pekee bali pia umeangalia jinsi ya kuunda maisha ya wanawake na kujenga mustakbali bora wa maisha kwa jamii za Afrika ikiwemo kuwainua wanawake na wasichana kwa kuwapa mikopo ya kuwawezesha kiuchumi.
Naye, Mwenyekiti wa Body wa “Merck Foundation” Prof. Frank Stangenberg-Haverkamp amesema, wakiwa wanasheherekea miaka 12 ya utekelezaji wa miradi yao mbalimbali, wanajisifia kwa kukuza ustawi wa watu kwa Afrika na Asia kwa ukubwa wake pamoja na mafanikio kwa programs zao zote.
Mtendaji Mkuu wa Merck Foundation Dr. Rasha Kelej ameeleza miongoni mwa shughuli nyingi wanazozifanya kwenye taasisi yao ni pamoja na kukabiliana na masuala ya udhalilishaji kwa wanawake, watoto na wasichana pamoja na kuwawesha kiuchumi na kujenga uelewa kwa jamii juu ya ustawi wao kupitia mitandao ya kidijitali.
Mkutano huo wa siku mbili umewakutanisha pamoja wake wa marais wa Afrika kutoka nchi 15, utaambatana na mafunzo kwa waandishi wa habari na washirika wake, ambapo watajadili pia kuhusu matumizi ya kidijitali kujenga uelewa kwa jamii juu ya kutambua uhalifu wa mitandao na kukomesha vitendo vya kikatili kupitia mitandao ya kijamii.