Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt, Hussein Ali vu Mwinyi amesema Serikali   itaendelea Kuimarisha Miundonbinu ya Sekta ya Elimu kwani ndio Kipaumbele cha kwanza cha Serikali anayoiongoza.Rais Dkt, Mwinyi ametoa Tamko hilo wakati wa Ufunguzi wa Skuli Tatu Mpya za Msingi za Ghorofa za Chumbuni, Kidichi na Skuli ya Msingi ya Abeid Amani Karume iliopo Mwera.

Rais Dkt, Mwinyi amefahamisha kuwa Serikali inajikita Kuimarisha Sekta ya Elimu kuanzia ngazi ya Msingi , Sekondari na Vyuo Viikuu kwani ni nyenzo Muhimu ya kufanikisha Maendeleo katika Sekta zote.Amebainisha kuwa kwa Muda mrefu Zanzibar ilikuwa ikikabiliana na Changamoto Tatu kuu katika Sekta ya Elimu ambazo Serikali imeamua kuziondosha.

Amezitaja Changamoto hizo kuwa ni Ukosefu wa Miundonbinu ya Elimu iliobora, Upungufu wa Walimu hususani wa Masomo ya Sayansi pamoja na Ukosefu wa Vifaa vya kufundishia na Kujifunza ambazo kwa Kiwango kikubwa zilidhorotesha Maendeleo ya Elimu hapa Nchini.Dkt, Mwinyi ameeleza kuwa Serikali itaendelea na Ujenzi wa Skuli za ghorofa katika maeneo mbalimbali pamoja na Kuongeza Idadi ya Walimu sambamba na Kuimarisha Maslahi Yao ili watekeleze Majukumu Yao kwa Ufanisi zaidi.

Aidha amefahamisha kuwa Serikali inakusudia kuzifanya Skuli zote kuwa na Viwango Bora vya kujifunzia kwa kuwa na Vifaa vya kutosha vya kujifunzia, Maabara, Maktaba na Vyumba vya Kompyuta Ili kuwaandaa Wanafunzi katika ngazi za awali.Rais Dkt, Mwinyi ameipongeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa Usimamizi Bora wa Ujenzi wa Skuli hizo Tatu pamoja na Uongozi wa Wilaya na Mikoa kwa Ufuatiliaji wa Miradi Hiyo.


Rais Dkt, Mwinyi amewahakikishia Wananchi kuwa kamwe hatayumbishwa na Kauli potofu za Watu Wasiopenda Maendeleo katika dhamira yake ya Kuleta Maendeleo na Mabadiliko katika Sekta ya Elimu.Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Lela Muhammed Mussa amesema Mageuzi Makubwa yanayoendelea katika Sekta ya Elimu yanasaidia Kuongeza Ufanisi katika Utekelezaji wa Mtaala Mpya wa Elimu na Ongezeko la Ufaulu wa Wanafunzi.

Akiwasilisha Taarifa ya Kitaaluma ya Ujenzi wa Skuli hizo Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Khamis Abdalla amesema kila Skuli imegharimu Kiasi cha Shilingi Bilioni 4.5 hadi kukamilika zikiwa na Madarasa 29 kila Moja Maabara, Maktaba na Vyumba vya Kompyuta.