RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Braza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema Serikali ina azma ya kuandaa mikakati madhubuti ili kufanikisha dhamira ya kuwa na uchumi endelevu wa bahari (Blue economy).
Hatua hiyo inakwenda sambamba na uimarishaji wa miundombinu ikiwemo ujenzi wa bandari kubwa ya kisasa, pamoja na kuwaelimisha wakulima hususan wale wa kilimo cha mwani.
Dk. Shein amesema hayo leo katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, wakati alipowasili akitokea nchini Kenya, alikohudhuria mkutano wa siku tatu wa Uchumi wa Bhari, akimuwakilisha Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Joseiph Pombe Magufuli.
Alipowasili uwanjani hapo, Dk. Shein na ujumbe wake walipokelewa na Viongozi mbali mbali wa chama na Serikali, akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa VIP, Dk. Shein alisema hatua hiyo ni kutekeleza kwa vitendo, miongoni mwa yale yaliofikiwa na nchi wanachama katika mkutano huo uliomalizika hivi punde.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari Dk. Shein alisema suala la mafuta na gesi asilia ni miongoni mwa neema za uchumi wa bahari, na kubainisha kuwa utafutaji wa nishati hiyo umeingia katika awamu ya pili ya utafiti katika eneo la maji madogo kisiwani Pemba.
Katika hatua nyengine, Dk. Shein aliwataka waandishi wa habari kuchukuwa nafasi yao katika kuwaelimisha wananchi juu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na athari za kiuchumi zinazojitokeza katika eneo la bahari ili kufanikisha dhamira ya kufikia uchumi wa viwanda.