RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameikaribisha Kampuni ya Al Nakhil kutoka nchini Dubai kuitumia fursa ya kuja kuekeza hapa Zanzibar katika sekta ya utalii. Dk. Shein alitoa maelezo hayo wakati alipofanya mazungumzo na Sheikh Ali Rashid Lootah Mwenyekiti wa Kampuni ya Al Nakhil kutoka nchini Dubai Ikulu mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alimueleza kiongozi huyo wa Kampuni kubwa ya ujenzi ya Al Nakhil ya nchini Dubai kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kutoa ushirikiano wake mkubwa na kuweka mazingira mazuri katika kuhakikisha azma ya Kampuni hiyo inafikiwa.  Dk. Shein alimueleza Mwenyekiti huyo kuwa Zanzibar ina fursa nyingi za uwekezaji katika sekta ya Utalii na iko tayari kutoa ushirikiano wake kwa Kampuni hiyo hasa ikizingatiwa kuwa ina uzoefu na uwezo mkubwa katika harakati hizo.

Aidha, Rais Dk. Shein alimueleza Mwenyekiti huyo juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya utalii sambamba na hatua zilizofikiwa katika kuhakikisha idadi ya watalii imeongezeka. Hivyo, Rais Dk. Shein aliendelea kusisitiza haja ya kuanzishwa kwa usafiri wa anga hasa kwa kutumia Kampuni ya ndege ya Emirates ambapo kati ya Zanzibar na Dubai, ambapo hatua hiyo itaimarisha na kuongeza idadi ya watalii na kuwasaidia wafanyabiashara na wasafiri wengine.

Alieleza kuwa tayari makampuni kadhaa ya ndege kutoka nchi mbali mbali duniani yamekuwa yakifanya safari zake Zanzibar na kusaidia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa sekta ya utalii hapa Zanzibar, hivyo kuna haja kwa Shirika hilo kufanya safari zake hapa Zanzibar. Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Mwenyekiti huyo wa Kampuni ya Al Nakhil kwa kuendelea kuiimarisha misikiti hapa Zanzibar hatua ambayo imewezesha kuikarabati misikiti pamoja na kuijenga mengine mipya.

Dk. Shein pia, alitoa pongezi kwa Mwenyekiti huyo kutokana na mapokezi makubwa aliyoyapata yeye na ujumbe wake wakati walipofanya ziara katika nchi za (UAE) na kutembelea katika eneo la mradi wa “Palm Jumairah” ambao unasimamiwa na Kampuni hiyo. Alieleza jinsi hatua za kuimarisha sekta ya utalii hapa nchini zinaendelea kuimarishwa ambapo pia, mikakati katika kuendelezwa na kuimarishwa sekta hiyo ilielezwa katika mkutano wa Uchumi wa Bahari ’Blue Economy’ uliomalizika hivi karibuni mjini Nairobi nchini Kenya.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumueleza Mwenyekiti huyo mikakati ya mashirikiano katika sekta za maendeleo iliyofikiwa katika mazungumzo kati yake na viongozi wa nchi za Falme za Kiarabu wakati alipokutana nao katika ziara yake ya nchi za (UAE) mapema mwaka huu.

Nae, Sheikh Ali Rashid Lootah Mwenyekiti wa Makampuni ya Al Nakhil kutoka nchini Dubai alipongeza hatua kubwa za maendeleo zilizofikiwa hapa Zanzibar sambamba na juhudi za makusudi zilizochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein katika kuimaisha sekta ya utalii. Sheikh Ali Rashid Lootah alitumia fursa hiyo kueleza jinsi alivyoshuhudia ongezeko la ujio wa watalii hapa Zanzibar na kuahidi kuwa licha ya Zanzibar kujiuza wenyewe kiutalii duniani lakini pia, atafanya juhudi za makusudi kuitangaza kutokana na fursa za kitalii zilizopo.

Aidha, alilipokea wazo la Rais Dk. Shein pamoja na mazungumzo aliyoyafanya na uongozi wa Kampuni ya ndege ya Emirates ya kufanya safari za ndege hizo kati ya Zanzibar na Dubai jambo ambalo litaongeza idadi ya watalii sambamba na kuwapa urahisi wafanya biashara na wananchi wanaosafiri kati ya pande mbili hizo. Alieleza kuwa kuwepo kwa mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo Zanzibar ikiwemo uwepo wa usalama na amani, ukarimu wa Wazanzibari pamoja na mikakati na Sera za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya utalii, vyote hivyo vimeivutia Kampuni yake kuja kuekeza hapa Zanzibar.

Mwenyekiti huyo alieleza kuvutiwa kwake na hatua za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuweka mradi wa mji salama katika maeneo ya mji wa Zanzibat ukiwemo Mji Mkongwe ambao ni kivutio kimoja wapo cha watalii wanaokuja kuitembelea Zanzibar. Pia, alipokea shukurani kutoka kwa Dk. Shein kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuiendeleza, kuikarabati na kujenga misikiti hapa Zanzibar na kuahidi kuendelea kwa lengo la kuiimarisha Uislamu.

Kampuni ya Nakhil ni miongoni mwa Kampuni kubwa nchini Dubai ambayo mbali ya ujenzi wa nyumba za makaazi pamoja na hoteli pia, inahusika na kurejesha ardhi kwa kufukia bahari ambapo kutokana na usarifu huo imeweza kujenga miradi kadhaa ukiwemo Palm Island, Dubai Waterfront, Visiwa vya The World, Visiwa vya Universe, Visiwa vya Jumeirah, ‘Jumerah lake Tower’, ‘Dragon Mart’, ‘Ibn Batuta Mall’ na miradi mengineyo ambayo ipo nchini humo.