Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za taasisi za kitaaluma za kimataifa zinazoonesha dhamira ya kushirikiana na Zanzibar kuijengea uwezo wa kielimu katika nyanja mbalimbali.

Dk.Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 13 Sept 2024 alipokutana na Mkuu wa Chuo kikuu cha Imperial cha Uingereza Profesa Lam Wamsley na Ujumbe wake Ikulu ndogo Mtaa wa Laibon Dar es Salaam.Aidha Dk.Mwinyi ameeleza kuwa bado nchi inahitaji kupanua wigo wa kitaaluma katika juhudi za kuleta Maendeleo kukuza Uchumi na kuongeza maarifa na Ujuzi wa watu wake.

Ameyataja maeneo ya biashara, afya, utafiti na teknolojia ya mawasiliano kuwa   muhimu kwa nchi na kuelezea kuunga mkono nia ya Chuo Kikuu cha Imperial cha Uingereza   ya kufungua milango ya ushirikiano wa kitaaluma na kuanzisha programu tofauti kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Suza.

Halikadhalika Dk.Mwinyi amesisitiza kuwa   Zanzibar imeendelea kuweka mkazo zaidi katika kuviimarisha Vyuo Elimu ya juu   ili kuandaa Wataalamu katika sekta mbalimbali na kwamba bado inahitaji kuungwa mkono   kimataifa.

Ujumbe huo umekuja nchini kuangalia maeneo ya ushirikiano na hatimae kuanzisha programu za mafunzo.