MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Hussein Ali Mwinyi ameiagiza Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufanyakazi ya uhamasishaji kuhakikisha Wanachama wa chama hicho wenye sifa wanajiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.Dk. Mwinyi ameyasema hayo, alipozungumza katika kongamano maalumu la Umoja wa Wazazi Tanzania la kupongeza juhudi za miaka minne ya uongozi wake na Serikali anayoiongoza ya awamu ya nane kwa maendeleo na mafanikio makubwa yaliyopatikana hapa nchini.
Aidha, Dk. Mwinyi ameutaka Umoja huo kuhakikisha WanaCCM watakaojitokeza kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapigakura, wanatumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura siku ya uchaguzi, 2025.Alifahamisha, kwa kufanya hivyo CCM, itakuwa na uhakika wa kupata wingi wa kura na ushindi mkubwa usio na mashaka na kuondosha malalamiko ya wapinzani kila wanaposhindwa uchaguzi.
Rais Dk. Mwinyi amesema, CCM ina kila sababu ya kushinda uchaguzi ujao wa 2025 kutokana na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho 2020 -2025 iliyovuka malengo katika sekta mbalimbali za maendeleo.Makamu Mweyekiti huyo wa CCM Zanzibar, amewasisitiza wanachama na viongozi wa jumuiya zote za Chama hicho kuendelea kujipanga vema na kufanyakazi za chama kwaajili ya uchaguzi mkuu ujao.
Alisema, CCM inaridhika na kazi inayofanywa na jumuiya ya wazazi na kutaka kuendelezwa ili kuwaunganisha wanachama kuwa na mwelekeo mmoja kwa dhamira ya kuendelea kuongoza nchi kwa miaka mingi ijayo.Pia, amepongeza uamuzi wa Jumuiya ya Wazazi kuandaa Kongamano maalum la kumpongeza kwa mafanikio ya miaka minne ya uongozi wake, na kuongeza kuwa hatua hiyo imemuongezea ari na motisha yeye na watendaji Serikalini ya kufanya mambo makubwa zaidi kuwaletea wananchi maendeleo.
Akizungumza kwenye Kongamano hilo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Fadhil Rajab Maganya, ameeleza kuwa Jumuiya itaendelea kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wagombea wote wa CCM wanashinda kwenye uchaguzi mkuu ujao pia ameelezea dhamira ya Jumuiya hiyo ya kujenga jengo la kisasa la ghorofa nne kwaajili ya ofisi za jumuiya hiyo katika eneo la sasa la ofisi ya Jumuiya hiyo.
Aidha, Jumuiya hiyo imekiomba Chama Cha Mapinduzi kuwaongezea idadi ya wajumbe wa viti maalumu kwenye mabaraza yao ya maamuzi.Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu CCM Taifa, Bal. Emmanuel Nchimbi, Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar, Muhamed Said Muhamed Dimwa, amesema CCM inaridhishwa na kiwango cha juu cha utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho unaofanywa na Serikali na kumuhakikisha Dk. Mwinyi kwamba, inaamini kuwa Dk. Hussein Mwinyi ndie atakaekuwa mgombea pekee wa chama hicho kwa nafasi ya Rais wa Zanzibar, 2025 hadi 2030.
Amesifu uongozi wa Dk. Mwinyi kwa kuendeleza jitihada za kuwaunganisha watu, maendeleo ya uchumi yanayonufaisha wananchi wote, kuzalisha ajira rasmi na siozo rasmi, kuajiri wataalamu wa fani zote, kuimarisha sekta ya huduma ikiwemo Afya, elimu na miundombinu ya maji na barabara za kisasa, viwanja vya ndenge Unguja na Pemba, Sekta ya Uchumi wa Buluu na kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa.
Naye, Mjumbe wa Halimashauri Kuu ya CCM, Taifa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema kazi inayofanywa na Dk. Mwinyi katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake imewaondoshea Wazanzibari matatizo kwa kiwango kikubwa katika nyanja mbalimbali za kijamii nakueleza kuwa kwa kuzingatia mafanikio hayo, Chama kinakusudia kuandaa mpango maalumu wa kuyaonesha mafanikio hayo kwa wananchi kuanzia ngazi ya wadi, Shehia, tawi hadi jimbo.
Kongamano hilo, lililokuwa na kauli mbiu “Mzazi mshike mwanao muhimize 2025 akapige Kura” liliandaliwa na Jumuiya ya Wazazi Tanzania ambayo imekua ya kwanza kufungua wiki ya kupongeza mafaniko ya miaka minne ya Serikali ya awamu ya nane ya uongozi wa Dk. Mwinyi.Jumiya hiyo pia ilimkabidhi Makamu Mwenyekiti wa CCM, Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi shilingi milioni 2.1 kwaajili ya kuchukulia fomu ya kugombea Urais wa Zanzibar wakati utakapofika na kupendekeza kwa Chama hicho kutoa fomu moja tu ya ugombea wa urais wa Zanzibar mwaka 2025.
Kwenye Kongamano hilo kuliwasilishwa mada mbalimbali zilizoeleza mchango wa Chama Cha Mapinduzi katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho, 2020-2025 ndani ya miaka minne ya uongozi wa Dk. Mwinyi, Mchango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kufanikisha utekelezaji wa Ilani hiyo, aidha, Mafanikio yaliyopatikana kwenye sekta zote za maendeleo ikiweo Elimu, Afya, Miundombinu ya maji, barabara, viwanja vya ndege, mawasiliano na Ustawi wa Wazee.