RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini juhudi za Jamhuri ya Korea za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya kilimo.
Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania Sog Geum-yong, ambaye amefika Ikulu kwa ajili ya kumuaga Rais baada ya kumaliza muda wake wa kazi hapa nchini.
Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alimueleza Balozi Sog kuwa Zanzibar inajivunia uhusiano na ushirikiano mwema uliopo kati yake na Jamhuri ya Korea ambao umeweza kusaidia kuimarika kwa sekta za maendeleo ikiwemo sekta hiyo ya kilimo ambapo tayari imejiandaa vizuri kwa kuweka mazingira mazuri ya mradi huo kwa kuyatayarisha mashamba yapatayo 60.
Rais Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa hatua za Jamhuri ya Korea kusaini mradi wa miundombinu ya kilimo cha mpunga wa umwagiliaji maji hivi leo ni uthibitisho wa wazi kuwa nchi hiyo imeamua kwa makusudi kushirikiania na Zanzibar kivitendo.
Alieleza kuwa tokea nchi hiyo ianze ushirikiano na ushusiano wa kidiplomasia kati yake na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar mnamo miaka ya tisini, imeweza kutoa ushirikiano wake mkubwa kwa Zanzibar kwa kuweza kusaidia miradi kadhaa ikiwemo kilimo, elimu, uvuvi na mengineyo ambayo imeweza kuimarisha sekta za maendeleo nchini.
Aidha, Rais Dk. Shein alieleza kuwa Jamhuri ya Korea imeweza kusaidia katika ujenzi wa skuli ya kisasa ya Sekondari ya Kwarara ambayo pia, ina studio ya matangazo pamoja na vifaa mbali mbali vya habari kwa ajili ya mafunzo na kutoa elimu kwa wananchi.
Pia, Rais Dk. Shein alieleza kuwa juhudi za Jamhuri ya Korea imeweza kusaidia kuanzishwa kwa kituo cha kutotolea vifaranga vya samaki (marine hatchery), kaa na majongoo ya baharini huko Bait el Ras ikiwa ni jitihada za kuhakikisha sekta ya uvuvi, ufugaji, ajira kwa vijana sambamba na ukuaji wa uchumi vinaimarika hapa Zanzibar.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa Jamhuri ya Korea imekuwa mshirika mzuri wa maendeleo ya Zanzibar kwa kuweza kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mikakati yake ya kupambana na umasikini pamoja na kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya 2020.
Rais Dk. Shein pia, alimtaka Balozi Sog kuitangaza Zanzibar kiutalii katika Jamhuri ya Korea sambamba na kuwakaribisha wawekezaji kuja kuekeza Zanzibar.
Aliongeza kuwa Zanzibar iko salama na ushahidi wa kuthibitisha hilo unaonekana pale Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilivyoamua kwa makusudi kuanzisha mradi wa mji salama ambao una malengo mazuri na mafanikio makubwa kwa wageni na wenyeji wa Zanzibar katika kuhakikisha amani na usalama wao unakuwepo muda wote.
Nae Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania Sog Geum-yong alimueleza Rais Dk. Shein kuwa Jamhuri ya Korea itaendeleza uhusiano na ushirikiano wake kati yake na Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mradi wa mpunga wa umwagiliaji maji unatekelezwa.
Alisisitiza kuwa katika kuongeza juhudi hizo kwenye sekta ya kilimo kupitia mradi huo uliosainiwa wa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji maji ambao unatarajiwa kuwa wa miaka mitatu utagharimu Dola za Kimarekani milioni 59.9.
Alieleza kuwa licha ya mradi huo kuchelewa kidogo lakini Jamhuri ya Korea bado ina imani kubwa kuwa utafanikiwa kutokana na azma iliyowekwa na nchi hiyo kwa Zanzibar hasa ikitambua juhudi za Rais Dk. Shein katika kuhakikisha Mapinduzi makubwa ya kilimo yanafanyika Zanzibar kupitia kilimo cha mpunga wa umwagiliaji maji.
Balozi Song alieleza kuwa mbali ya mradi huo wa mpunga wa umwagiliaji maji tayari nchi yake kupitia Mashirikika yake likiwemo Shirika la Maendeleo la Jamhuri ya Korea (KOICA) linaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi mbali mbali hapa Zanzibar.
Aidha, Balozi huyo alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa kutokana na mafanikio makubwa iliyofia Zanzibar katika sekta ya utalii atahakikisha anaendelea kuitangaza kiutalii kutokana na kuwepo vivutio kadhaa ambavyo ni adimu kuvipata katika maeneo mengine duniani.
Pia, Balozi huyo ameahidi kuimarisha mashirikiano na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) katika kuendeleza programu mbali mbali sambamba na kusaidia Dola za Kimarekani milioni 10 kwa ajili ya Mradi wa kusaidia elimu ya Sekondari ambao utajumuisha ujenzi wa vituo vya kufundishia Sayansi na Maktaba kwa ngazi ya elimu ya Sekondari pamoja na mradi wa mafunzo kwa walimu kazini.
Balozi Sog alitumia fursa hiyo kumpongeza na Rais Dk. Shein na Serikali anayoiongoza kwa kumpa mashirikiano makubwa wakati wote alipofanya kazi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar.