RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amewataka akinamama kote nchini kupeana elimu juu ya umuhimu wa kuchunguzwa saratani ya shingo ya kizazi pamoja na kuwataka watoto wa kike kuhudhuria vituo vya afya kupata chanjo ya maradhi hayo.
Amesema hatua hiyo itawezesha kugundulika mapema viashiria vya kuwepo maradhi hayo na hivyo kuweza kupata tiba sahihi na kwa wakati muafaka. Dk. Shein amesema hayo leo katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa uchunguzi wa Saratani ya shingo ya kizazi, iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-wakil, Kikwajuni mjini hapa. Mradi huo wa miaka minne unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kupitia Wizara ya Afya pamoja na Kamisheni ya Afya na uzazi wa mpango, kutoka Jimbo la Jiangsu nchini China.
Hafla hiyo imewashirikisha viongozi mbali mbali wa Serikali, madaktari; wauguzi na wataalamu kutoka sekta ya afya, wawakilishi wa Kamisheni ya Afya na mpango wa uzazi kutoka Jiangsu pamoja na wadau wengine wa sekta ya Afya nchini. Dk. Shein alisema kuna umuhimu mkubwa kwa akinamama kuhimizana na kupeana elimu, ili kila mmoja aone umuhimu na faida ya kwenda kuchunguzwa maradhi hayo, sambamba na kuwahimiza watoto wa kike walio na umri kati ya miaka tisa hadi 14 kupata chanjo kama inavyoelekezwa na wataalamu. Alisema katika kufanikisha jambo hilo, ni muhimu kwa akinababa kuiunga mkono jinsia hiyo ili kuepukana na athari mbali mbali zinazoweza kujitokeza, ikiwemo uchelewaji wa kupata matibabu.
“Nyenzo zipo na wataalamu wapo, hivyo vyema tuzingatie usemi usemao tusifuge ndwele na waganga tele, hakuna sababu ya kuona haya, wajitokeze katika uchunguzi, tukiona aibu tutaharibu nafasi ya kuchunguzwa’, alisema.
Alieleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadhamini wa mpango huo watawahudumia na kuwapatia matibabu sahihi na kwa wakati muafaka wale wote watakaobainika kuwa na matatizo, hatua hiyo ikiwa ni kuzingatia sera ya Serikali ya kutowa matibabau bure kwa wananchi bila ya ubaguzi.
Aidha, alisema mpango huo unakwenda sambamba na azma ya serikali ya kuhakikisha huduma za afya zinaendelea na ustawi wa afya ya wanawake unaimarika, kama ilivyohimizwa katika Ilani ya CCM ya 2015- 2020.
“Tumedhamiria kuongeza kasi katika kuhakikisha huduma muhimu za afya zinatolewa hapa hapa nchini, ili kuwapunguzia usumbufu wananchi pamoja na kupunguza gharama za matibabu za kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi”, alisema.
Dk. Shein aliitaka jamii kuendelea kushirikiana na Wizara ya Afya ili kufanikisha mpango huo, akibainisha kuwa una umuhimu wa pekee na utawezesha kujua taarifa halisi za ukubwa wa maradhi hayo hapa Zanzibar. “Lakini pia utatuwezesha kujua mwenenndo na aina ya virusi vya HPV hapa Zanzibar kwani ndivyo vinavyosababisha kupatikana saratani hiyo kwa asilimia 90’, alisema.
Dk. Shein alieleza kufarijika na kampeni iliyofanywa na Serikali ya kuwapatia chanjo dhidi ya ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi watoto wa kike wenye umri wa kuanzia miaka tisa hadi 14, ambapo uzinduzi wake ulifanyika April, mwaka huu. Alisema kampeni hiyo iliyowashirikisha washirika wa maendeleo kutoka Mashirika ya WHO,UNICEF na mengineyo Duniani imetowa mwanga katika kunusuru maisha ya wanawake wengi hapa nchini.
“Kwa mantiki hiyo naendelea kusisitiza bado suala la kinga linahitaji kupewa umuhimu mkubwa mno katika kukabiliana na maradhi haya, tusisubiri hadi yajitokokeze na kuanza kutuathiri na ndipo tuanze kuchukua hatua’, alisistiza. Akigusia ukubwa wa tatizo hilo, Dk. Shein alisema ugonjwa huo thakili umekuwa ukipoteza roho za watu wengi hapa nchini na kubainisha kuwa taasisi ya Saratani ya hospitali ya Ocean Road imeripoti kuwa jumla ya wanawake 35,000 hupata saratani ya shingo ya kizazi kila mwaka, huku asilimia 20 pekee ndio hufika katika taasisi hiyo kwa matibabu.
Aidha, alisema takwimu za maradhi hayo katika Kilinik ya Hospitali ya Mnazimmoja inaonyesha kuwa asilimia 80 ya wanawake wenye aina hiyo ya saratani, hufika hospitali kwa ajili ya matibabu, wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa huo.
Katika hatua nyengine, Dk. Shein alikemea vikali tabia ya baadhi ya watendaji katika sekta ya Afya ya kufanya kazi bila kuzingatia maadili ya kazi zao. Alisema utekelezaji wa mradi huo, utaweza kufanikiwa vyema, endapo tu watendaji watatekeleza vizuri dhamira za kufanya uchunguzi wa saratani ya shingo ya kiazazi kwa kuzingatia uwezo wa kiuchumi wa nchi pamoja na mila na desturi za wananchi wa Zanzibar. Aliwakumbusha madktari, wauguzi na watendaji wote wa sekta hiyo kuzingatia suala la maadili ya kazi katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Wizara lazima iwe makini katika kuhifadhi na kulinda taarifa na siri za wagonjwa ili wananchi wazidi kuzipokea vizuri juhudi zetu za kutoa kinga ya maradhi mbali mbali, siri ya mgonjwa ni kati ya mgonjwa mwenyewe na Daktari’, alifafanua.
Akinasibisha kauli yake na matukio yaliojiri duniani katika siku za hivi karibuni, Dk. Shein alisema, dharau, sahau, kubabaika na kutozingatia maadili ya kazi kwa daktari au muuguzi, sio tu kuwa kunaharibu sifa za mtu huyo, bali kwa kiasi kikubwa kunaathiri sifa za taasisi na baadhi ya nyakati, nchi nzima.
Aidha, Dk. Shein aliwataka Viongozi wa Wizara hiyo pamoja na Vituo vya Afya kote nchini kuzingatia upya suala zima la matumizi ya simu za mkononi na nyenzo nyengine za mawasiliano ya kiasa yanayofanyika katika Wodi za Hospitali pamoja na maeneo yote muhimu yanayohifadhi na kulinda siri na taarifa za wagonjwa.
“Ipo haja ya kuangalai upya ni maeneo gani tuyaruhusu, ili wafanyakzi na wagonjwa waingie na simu na nyenzo nyengine zinazotumika kutoa taarifa, suala la maadili ni pana mno , hivyo viongozi wa afya mnapaswa mlizingatie katika mpango huu”,alisema.
Vile vile, aliutaka uongozi wa Wizara hiyo kubuni mipango kabambe itakayowezesha kuendeleza mpango huo baada ya kipindi cha ufadhili (miaka minne) kumalizika, ili mafanikio yatakayopatikana yawe endelevu.
Mapema, Balozi mdogo wa China, Xie Xiaowu alisema China itaendeleza ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati yake na Zanzibar katika sekta ya afya, ambapo kwa nyakati tofauti imekuwa ikitowa msukumo katika nyanja mbali mbali, ikiwemo afya ya jamii, ujenzi wa miundo mbinu, uaptikanaji wa vifaa pamoja na wataalamu.
Nae, Waziri wa Afya Zanzibar, Hamad Rashid Mohamed alisema ujio wa mradi huo utafanikisha azma ya Serikali ya kuwa an wanawake imara na wenye afya njema.
Alisema wanawake wanakabiliwa na changamoto mbali mbali za maradhi, ikiwemo saratani ya shingo ya kizazi, hivyo akawataka akinamama kutumia vyema fursa hiyo, ambapo watachunguzwa na kupatiwa tiba bila ya malipo yoyote.
Aidha, Naibu Rais kutoka Naijing Drum Tower Hospital, alisema mradi wa uchunguzi wa shingo ya kizazi, ni eneo jipya la ushirikiano katika sekta ya afya, kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Jimbo la Jiangsu nchini China.
Alisema katika kukabiliana an saratani ya shingo ya kizazi, suala la elimu ya kina linalopaswa kupewa umuhimu pamoja na kufanyika uchunguzi kabla ya tiba.
Nae, Katibu Mkuu wa Wizara Afya, Asha Abadalla alipongeza uongozi wa kamisheni ya Afya na uzazi wa mpango kutoka jimbo la Jiangsu nchini China , kwa utayariwao katika utekelezaji wa mpango huo.
Uchunguzi wa saratani ya shingo ya Kizazi hufanyika kwa wnaawake wenye umri wa kunzia miaka 21 hadi 65, ambapo wastani wa wanawake 35,000 wanatarajiwa kuchunguzwa katika kipindi hicho na kupatiwa matibabu na Serikali.