RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametembelea eneo la Mpigaduri linalotarajiwa kujengwa bandari mpya pamoja na eneo la Kinazini linalotarajiwa kujengwa mji wa kisasa ikiwa ni miongoni mwa juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukuza uchumi na kuimarisha maendeleo na ustawi wa jamii.Akiwa amefuatana na viongozi mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd pamoja na Wajumbe wa Baraza la Mapinduzi, Rais Dk. Shein alifanya ziara hiyo fupi ya kutembelea maeneo hayo ambayo yametengwa maalum kwa miradi hiyo ya ujenzi wa bandari mpya pamoja na mji mpya wa kisasa.
Dk. Shein alitembelea maeneo hayo ambayo yametengwa maalum kwa miradi hiyo ambayo ujenzi wake ni miongoni mwa juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufungua milango zaidi ya kiuchumi sambamba na kuleta maendeleo endelevu kwa Zanzibar na wananchi wake.Akiwa katika ziara hiyo Dk. Shein aliziagiza mamlaka na taasisi zinazohusika na eneo la pembezoni mwa bahari linaloanzia Bwawani, Mpigaduri hadi Maruhubi kuharakisha matayarisho ya eneo hilo, ili kupisha utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Bandari ya Mizigo utakaofanywa na Kampuni ya Kimataifa ya Uhandisi inayoshughulikia miradi ya Ujenzi wa Bandari na Madaraja Makubwa ya China (CHEC).
Pia, Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kusisitiza haja kwa Taasisi husika kuwatafutia ufumbuzi wa haraka wananchi wanaofanya shughuli zao katika eneo hilo litakalojengwa bandari mpya kwa kuwapatia eneo maalum lililotengwa huko Kihinani Wilaya ya Magharibi “A” ili kuepuka msongamano wakati wa kuanza kwa mradi huo.Utekelezaji wa mradi huo wa Bandari mpya ya Mpigaduri unatokana na mazungumzo aliyoyafanya Rais Dk. Shein na Rais Xi Jinping wa China wakati wa ziara yake nchini Tanzania na baadae Dk. Shein alipofanya ziara nchini China ambapo suala hilo lilizungumzwa kwa kirefu na matokeo yake ndio utekelezaji wa mradi huo hivi sasa.