RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amezishauri Taasisi za Elimu ya juu ziliopo nchini kuanzisha Kozi muhimu zenye uhitaji na uhaba wa Wataalamu zitakazochangia maendeleo ya nchi.Rais Dk. Mwinyi ameeleza, hatua hiyo itaisaidia Sekta ya afya kuwa na Wataalamu wa kutosha katika kada mbalimbali watakaotoa huduma kwa kuzingatia utaalamu na weledi na kuimarisha sekta ya afya.

Rais Dk. Mwinyi ametoa tamko hilo leo tarehe 19 Oktoba viwanja vya Mao Tse Tung kwenye Mahafali ya 12 ya Zanzibar School of Health.Rais Dk. Mwinyi ametoa wito kwa wahitimu wa kada tofauti kuzingatia nidhamu na maadili ya kazi katika utoaji wa huduma wanapoingia kwenye majukumu yao na kuwa msaada muhimu kwa jamii.

Aidha, amewasisitiza vijana kusoma kozi zenye umuhimu na uhitaji hususani mpya zinazoanzishwa na Zanzibar School of Health na kuongeza juhudi zinazochukuliwa na Chuo hicho kuanzisha kozi mpya.Rais Dk. Mwinyi amewahakikishia wamiliki wa Zanzibar School of Health kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono malengo ya Chuo hicho ya utoaji wa taaluma bora na juhudi ya kuelekea kuwa Chuo kikuu cha Afya hapa nchini.

Rais Dk. Mwinyi amefahamisha kuwa juhudi hizo zinaendana na malengo ya Serikali ya kuona Chuo hicho kinakuwa chem chem ya kuzalisha Wataalamu katika sekta Afya.Dk. Mwinyi ametoa wito kwa wahitimu kutoridhika na Elimu walioipata bali kutafuta fursa zaidi za Elimu ya juu kuziongezea maarifa na ujuzi.

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwnyi alizindua Stashahada ya usimamizi wa mfumo wa taarifa za Afya na Stashahada ya uchunguzi wa macho.Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Moh’d Mussa ameipongeza taasisi hiyo kwa kuendelea kuzalisha Wataalamu wa kada mbalimbali katika sekta ya Afya, hatua alioielezea kuwa ni muhimu kwa ustawi wa jamii na kuimarisha huduma ya Afya.

Amefahamisha, hatua ya kuanzisha kozi mpya itaisadia nchi kuwa na Wataalamu wa kutosha katika kada tofauti na kuahidi kwa Wizara kuunga Mkono.Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Zanzibar School of Health, Aziza Omar Hemedi ameeleza kuwa Wahitimu wa Chuo hicho wamekuwa nguzo muhimu ya utoaji wa huduma za afya katika Vituo vya Afya kwa Wananchi.

Amefahamisha, Chuo hicho kimeanzisha kozi mpya tatu ikwemo Stashahada ya Usimamizi wa Majanga, Stashahada ya Uchunguzi wa macho na kozi ya Stashahada ya Ushauri nasihi.Jumla ya wahitimu 640 wa kada mbalimbali wamehitimu na kutunukiwa vyeti na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Chuo hicho, tayari kimezalisha wahitimu 3000, tangu kuanzishwa kwake mwaka 2011 ambapo wametawanyika kwenye taasisi mbalimbali za Umma na Binafsi kwaajili ya kutoa huduma.