RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka viongozi na wafanyakazi wa Shirika la Magazeti ya Serikali kuendelea kuwa wabunifu katika kuandika habari na hasa zile zinazogusa maisha ya kila siku ya wananchi.Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo katika sherehe za kutimiza miaka 20 ya Gazeti la Zanzibar Leo, zilizofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip, huko katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Kiembesamaki Zanzibar.

Sambamba na hatua hiyo, Rais Dk. Mwinyi aliwahimiza viongozi na wafanyakazi hao wa Shirika la Magazeti kwenda na kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia ambayo imeongeza ushindani katika sekta ya habari kama ilivyo katika sekta nyengine.Aliongeza kuwa miongoni mwa majukumu ya msingi ya Gazeti la Serikali la Zanzibar leo ni kutoa taarifa sahihi, kwa wakati, na zenye ubora ili kukabiliana na ushindani uliopo hasa kutoka kwa magazeti ya kampuni binafsi.

“Kwa mnasaba huo uongozi na wafanyakazi wa gazeti hili mnapaswa kufanya kazi zenu kwa weledi ili kuwafanya wananchi na wasomaji wote waweze kuliamini gazeti letu kuwa ndicho chombo kinachotoa taarifa sahihi zilizoandikwa kwa umakini na zilizofanyiwa uchunguzi”alisema Dk. Mwinyi.Katika hotuba yake hiyo, Rais Dk. Mwinyi alikumbusha kwamba vyombo vya habari vya Serikali ni mdomo wa Serikali kwa hivyo vina wajibu mkubwa wa kuisemea Serrikali.

Alisema kuwa kutokana na kukua kwa tasnia ya habari na maendeleo ya sayansi na teknolojia duniani, wapo baadhi ya watu huitumia vibaya fursa hiyo kwa kupotosha habari hivyo, vyombo vya habari vya serikali vina jukumu la kuchukua hatua za haraka za kuelezea usahihi wa taarifa yenyewe kwa kutumia hoja, vielelezo na ufafanuzi wa jambo lenyewe.Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwapongeza Mawaziri wote kwa kutoa taarifa za kina juu ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara zao katika kipindi cha maadhimisho ya miaka 58 ya Mapinduzi na kutoa wito kuwa waendelee na utaratibu huo na usiwe katika kipindi cha sherehe pekee.

Aidha, aliwataka viongozi na watendaji wa taasisi mbali mbali za Serikali kuvitumia vyombo vya habari vya umma pamoja na vya binafsi kutoa taarifa za utekelezaji wa mipango mbalimbali ya Serikali kwa umma, kubainisha changamoto pamoja na kueleza namna watakavyokabiliana na changamoto hizo.Alieleza kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa uongozi na watendaji wa Shirika la Magazeti katika kuimarisha mazingira ya kufanya kazi pamoja na kuzifanyia kazi changamoto wanazozikabili huku akitumia fursa hiyo kutoa agizo kwa taasisi za Serikali na sekta binafsi zinazodaiwa na Shirika hilo kulipa madeni yao ili Shirika hilo liweze kuendesha shughuli zake.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Awamu ya Saba kwa kuwekeza fedha nyingi katika kuimarisha sekta ya habari hapa Zanzibar.

Nae Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita alitoa pongezi kwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Sita Dk. Amani Abeid Karume kwa kuwa muasisi wa Gazeti hilo pamoja na Rais Mstaafu wa Awamu ya Saba Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuliendeleza na kuipa msukumo mkubwa sekta ya habari kupitia vyombo vya umma likiwemo gazeti hilo.Sambamba na hayo, Waziri Tabia alitoa pongezi kwa Rais Dk, Mwinyi zinazotoka kwa wadau mbali mbali kutokana na uwamuzi wake wa kuzungumza na waandishi wa habari kila mwisho wa mwezi.  Pia, Waziri Tabia alitumia fursa hiyo kuwapongeza wafadhili wote waliofadhili shughuli hiyo ambayo ilifana.

Nae Mhariri Mtendaji wa Gazeti la ZanzibarLeo, Ali Haji Mwadili akisoma risala ya kitaalamu ya Shirika la Magazeti ya Serikali alisema kuwa gazeti hilo lililoanzishwa tarehe 12 Januari 2022 na Rais Mstaafu wa Awamu wa Sita Amani Abeid Karume likichukua nafasi ya Gazeti la Wiki la NURU.Alisema kuwa malengo ya kuanzishwa kwa gazeti hilo ni kusambaza Serta za Serikali kwa wananchi na kuwa kiungo muhimu kati ya wananchi na Serikali yao sambamba na kusambaza habari za kutosha, za kweli, uhakika na kwa wakati kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Aliongeza kuwa kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni “Habari na Uchumi wa Buluu” yenye lengo la kukumbusha umhimu wa na mchango wa sekta ya habari katika maendeleo na mafanikio ya uchcumi wa buluu kwa kuwaelimisha na kuwahabarisha wananchi.Akieleza miongoni mwa mafanikio Mhariri Mtendaji huyo alieleza kuwa ndani ya miaka 20 Gazeti al ZanzibarLeo limezaa magazeti mengine manne ambayo ni Zanzibar Leo Jumaapili,Zasport, Zanzibar Mail pamoja na Zanzibar Leo wanawake linalochapishwa kila mwisho wa mwezi huku likipanua wigo wa usambazaji magazeti kwa mikoa 11 ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Aidha, alieleza changamoto zinazolikabili gazeti hilo ikiwa ni pamoja na kupanda kwa gharama za uchapishaji na usambazaji wa magazeti kutokana na kupanda kwa malighafi na wakati mwengine wachapishaji kutaka faida kubwa ambapo kwa sasa asilimia 70 ya mapato ya Shirika yanatumika katika uchapishaji.Alisema akuwa kutokana na maendeleo ya kimtandao na mabadiliko ya tasnia ya habari, magazeti duniani yanahitajika kuendana na matakwa hayo ambapo kwa sasa shirikalinajipanga kuimarisha mitandao yake na kuendelea kuuza magazeti yake wka njia ya mtandao. 

Katika sherehe hiyo pia, Rais Dk. Mwinyi alizindua tovuti ya muonekano mpya wa gazeti la Zanzibar Leo (layout) pamoja na kutoa zawadi kwa watendaji wa Shirika wakiwemo Wenyeviti wa Bodi waliopita na wapya, Wahariri Watendaji waliopita na aliopo.Aidha, Rais Dk. Miwnyi alipewa zawadi ambapo pia, alikabidhi zawadi kwa Marais wastaafu akiwemo Dk. Karume na Dk. Shein pamoja na kumkabidhi zawadi waziri wa Wizara hiyo Tabia Maulid Mwita.

Burudani mbali mbali zilikuwepo katika hafla hiyo ikiwa ni pamoja na kikundi cha Zanzibar One Modern Taarab kilichoimba nyimbo kadhaa ukiwemo wimbo maalum wa miaka 20 ya Gazeti la Zanzibar Leo pamoja na wasanii kutoka kisiwani Pemba walioimba wimbo maalum wa kumpongeza Rais Dk. Mwinyi.