RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar inahitaji kuungwa mkono zaidi hasa kwenye eneo la utaalamu, miundombinu na kuwajengea uwezo watendaji wa sekta ya afya ili kutoa huduma bora kwa wananchi.Dk. Mwinyi ameyasema hayo Ikulu Zanzibar, alipozungumza na timu ya madaktari bingwa kutoka taasisi ya Umoja wa Madaktari bingwa wenye asili ya India wanaoishi Marekani (GAPIO) kuelezea dhamira yao ya kushirikina na Serikali kuimarisha sekta ya Afya katika maeneo mbalimbali.

Rais Dk. Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inaendelea na ujenzi wa miundombinu ikiwemo hospitali za Wilaya na vituo vya Afya kwa maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba ili kuhakikisha wananchi wanapata matibabu bora.Hata hivyo, amewaeleza madaktari hao kwamba bado kuna pengo linalohitaji kufanyiwa kazi ili kufikia malengo ikiwemo, upatikanaji wa vifaa tiba na dawa za kutosha, rasilimaliwatu, fedha hasa katika usimamizi wa Bima ya Afya na miundombinu kwenye sekta ya Afya.

Akizungumzia kuanzishwa kwa bima ya Afya kwa wenyeji na wageni wanaoingia nchini, Dk. Mwinyi amesema inasaidia fedha za uendeshaji kwa Sekta ya Afya akitolea mfano watalii 18 ambao wamenufaika na bima ya afya.Aidha, amesema Serikali inakusudia kuimarisha huduma za bima ya Afya kwa njia ya kidigitali ili kurahisisha wageni kupata huduma hiyo hata wakiwa nje ya Zanzibar.

Alisema, kuna haja ya kuangalia mfumo mzima wa Sekta ya Afya licha ya kujengwa hospitali 11 za Wilaya, bado kuna changamoto zimejitokeza ikiwemo uhaba wa wataalamu kwenye hospitali hizo, vifaa tiba na dawa na teknolojia ndogo.Kuhusu rasilimaliwatu, Rais Dk. Mwinyi aliwaeleza wataalamu hao kuangalia zaidi uwezekano wa kuwawesha kiutaalamu na mfumo mzima wa uendeshaji wa sekta ya Afya, Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi, ameihakikisha timu ya madaktari hao kuwa Serikali ipo tayari kushirikiana nao kwa kuandaa mazingira rafiki yakufanyakazi pamoja na ukaribu zaidi kwa kuwa na mipango ya muda mfupi, wakati na muda mrefu ili kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali kupitia wizara ya Afya na taasisi ya GAPIO.

Mratibu wa ujio wa madaktari hao kutoka hospitali ya Apolo ya Dar es Salaam, Dk. Nazir Arab amesema lengo ya taasisi yao ni kusambaza madaktari zaidi ya 1.4 milioni duniani, Tanzania ikiwemo Zanzibar kuwa miongoni mwa nchi zitakazofikiwa.Amesema hadi sasa taasisi ya GAPIO inawakilishwa ndani ya nchi 57 duniani hasa kwa mataifa ya Mashariki ya mbali, kusini Mashariki mwa bara Asia na Afrika ikiwa na lengo la kuimarisha sekta ya Afya duniani kote.

Timu hiyo ya madaktari bingwa 20 ikiongozwa na Prof. Sanku Rao wakifuata na Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya kutoka Wizara ya Afya, Dk. Salim Slim na timu ya watendaji ya Wizara hiyo, watakuwa na vikao vya pamoja vya kubainisha maeneo ya ushirikiano hasa katika magonjwa na Wataalamu wa upasuaji wa maradhi ya moyo, matumbo ya kawaida na matumbo ya wanawake, maradhi ya mifupa, wataalamu wa magonjwa ya watoto, wazee na wanawake, magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo sukari, presha na moyo.