RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapindizi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kusimamia hifadhi za barabara na kuwazuia wananchi kutojenga na kufanya biashara maeneo hayo ili kukwepa mzigo mkubwa wa fidia kwa Serikali pale inapotaka kupitisha miundombinu mengine muhimu.

Amefahamisha kuwa hivi sasa kumezuka tabia ya wananchi kuzitumia hifadhi za barabara kwa kujenga na kufanya biasharara bila kujali umuhimu wa hifadhi hizo na wakati mwengine kuziathiri barabara zilizojengwa.Dk. Mwinyi ametoa agizo hilo alipofungua barabara mpya ya Jozani, Charawe, Ukongoroni hadi Bwejuu, Mkoa wa Kusini Unguja yenye urefu wa kilomita 24.5.

Ameeleza kuwa wananchi wanawajibu mkubwa wa kutunza barabara zinazojengwa katika maeneo yao, kuonesha kuthamini juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali kuwajengea miundombinu bora ya usafiri na kuwaondoshea usumbufu waliokuwa wakiupata siku za nyuma.Aidha, amewahakikishia wananchi kwamba Serikali itaendeleza ujenzi wa miundombinu ya barabara nchi nzima na kuwasisistiza kuunga mkono juhudi hizo.

Rais Dk. Mwinyi amewathibitishia wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja kuwamalizia barabara ya Tunguu - Makunduchi kwa kiwango cha njia nne zenye taa kutoka Mwanakwerekwe hadi Makunduchi.Akizungumzia tatizo la maji kwa mkoa huo, Rais Dk. Mwinyi, amesema tayari Serikali imejenga skim nne kuu za maji safi ambazo zitamaliza tatizo la maji mkoani humo.
Kuhusu tatizo la umeme mdogo katika mkoa huo, amesema Serikali inatambua kwa muda mrefu kuwepo kwa tatizo hilo katika eneo hilo na kwamba imeshanunua “Grid Stabilization” na amefarajika kusikia tatizo hilo limeanza kupungua katika baadhi ya maeneo ya Mkoa huo.

Pia Dk. Mwinyi amemridhia ombi la Wananchi wa Kusini la kujengewa daraja lililoombwa na wananchi wa mkoa huo, litalounganisha Mkoa huko na wa Kaskazini Unguja lengo ni kurahisisha Mawasiliano baina ya mikoa miwili hiyo na huduma nyengine za uchumi na jamii.Alibainisha kuwa tayari msanifu amekamilisha michoro na kuiwasilisha kwa Serikali kwa hatua za awali na kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali inasubiri kujua gharama ili hatimae kulijenga daraja hilo.

Akigusia sekta ya Elimu Rais Dk. Mwinyi amewaahidi wananchi wa Zanzibar kuwa awamu ya pili ya ujenzi wa skuli za ghorofa 26 unakuja na Mkoa wa Kusini Unguja utakuwa miongoni mwao.Mapema akiwasalimia wananchi wa Kijiji cha Charawe, Rais Dk. Mwinyi amewasisitiza kutumia fursa za kuwepo kwa barabara hiyo kujinufaisha kiuchumi nakuwaeleza kuwa itawarahisishia kusafirisha kwa wakati bidhaa wanazozizalisha pamoja na kupata huduma nyengine kwa haraka.

Akizungmza kwenye hafla hiyo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema kufunguliwa kwa barabara hiyo ni kichocheo cha kufungua fursa za kiuchumi Mkoani humo pia Serikali inakwenda kutekeleza miradi mengine 162 katika sekta za maji, afya, elimu na barabara nchi nzima kuelekea maadhimisho ya miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Naye, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Dk. Khalid Muhamed Salum, amesema, Zanzibar imeingia kwenye ramani ya dunia katika ujenzi wa haraka wa miundombinu kutokana na juhudi na kazi kubwa zinazofanywa na Rais Dk. Mwinyi ndani ya kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya nane