RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameiagiza Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, kuandaa mkakati maalum utakaovutia na kuleta mashindano ya michezo mbalimbali nchini ili viwanja vilivyojengwa kutumika ipasavyo.

Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo alipozindua awamu ya pili ya Uwanja wa “Amani Sports Complex,” Mkoa wa Mjini Magharibi,  uliojumuisha miradi mbalimbali ikiwemo hoteli inayokaribiana na hadhi ya nyota tano, mkahawa wenye hadhi ya kimataifa, maegesho ya magari, maduka na viwanja mbalimbali vya michezo (In door games) ya Judo, Ngumi, mpira wa kikapu (basketi ball), mpira wa wavu, (volleyball), mpira wa mikono (hand ball) na mchezo wa “long tennis”, ikiwa ni muendelezo wa shamrashamra za miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

“Ni lazima kuandaa mashindano makubwa ili viwanja hivi kutumika ipasavyo” alisisitiza, Rais Dk. Mwinyi.Pia, Rais Dk. Mwinyi amehimiza kutumiwa kwa kumbi za mikutano zilizomo kwenye uwanja wa huo kwa mikutano ya ndani na ya kimataifa pamoja na kutoa wito kwa wananchi kuzitumia fursa zinazopatikana viwanjani hapo kwa kushiriki michezo hiyo kwa lengo la kujiongezea tija na kukuza sekta ya michezo nchini.

Dk. Mwinyi ameeleza kuwa Zanzibar ina kila sababu ya kujivunia kwa kuwa na viwanja bora vyenye viwango vya kisasa vya kimataifa.Amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu ya nane imeiweka Zanzibar kwenye viwango vya kimataifa, hasa linapokuja suala la michezo kwamba itazidi kujibebea hadhi ya kimataifa kwa kuwa na viwanja vyenye hadhi ya juu kila eneo.

Akizungumzia michuano ya AFCON ambapo Tanzania wa kushirikiana na Kenya na Uganda wanatarajiwa kuwa wenyeji wa mashindano hayo, Rais Dk. Mwinyi ameeleza kuwa Zanzibar ikiwa Sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejiandaa kwa mashindano hayo kwa kujenga miundominu yenye hadhi ya kimataifa kama mwenyeji wa mashindano hayo.Amesema, kuelekea AFCON Zanzibar itaunda kamati maalum ya kitaifa itakayosimamia michuano hiyo kwa mafanikio makubwa.

Hafla ya uzinduzi wa awamu ya pili ya Uwanja wa “Amani Sports Complex,” iliambatana na Sherehe maalum ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Mhe. Rais Dk. Mwinyi iliyoenda sambamba na ukataji wa keki na wimbo maalum wa kumpongeza kuzaliwa kwake.Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Tabia Maulid Mwita amesema kazi kubwa inayofanywa na Awamu ya nane ya Serikali ya Mapindizi ya Zanzibar imeiheshimisha Zanzibar na watu wake hasa katika kuimarisha miundominu ya kisasa ya michezo.

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana amempongeza juhudi za Serikali kwa Maendeleo makubwa yanayoendelea Zanzibar.Naye, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Fatma Hamad Mbarouk, amesema kinachofanyika kwenye sekta ya michezo nchini ni uimarishaji wa miundombinu imara katika kukuza tasnia ya michezo, hatua aliyoielezea kwamba itaweka historia itakayokubukwa wakati wote na jamii.

Aidha, ameongeza kuwa Wizara ya Habari pia itaendelea kusimamia miongozo na maelekezo wanayopokea kwa Rais Dk. Mwinyi kwa nia ya kuleta maendeleo zaidi na kuimarisha usatawi wa jamii kupitia michezo.Kwa upande wake Mkandarasi Kutoka kampuni ya Orkun ilifanikisha miradi hiyo, wameishukuru Serikali ya Mapindizi ya Zanzibar kwa kuwaamini na kuwakabidhi kazi kubwa wanayojivunia kuikamilisha na kuikabidhisha kwa Serikali kwa wakati.