RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amehudhuria msiba wa aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Marehemu Bi. Thereza Olban Ali nyumbani kwake Miembeni, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.Dk. Mwinyi ametoa salamu za pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki.Marehemu Bi. Thereza Olban alikua wanne kuzaliwa kwenye familia ya Shemasi Olban Ali na Bi. Christina Merry Ali, alizaliwa tarehe 15, Oktaba mwaka 1943 Mkunazini, Zanzibar.
Marehemu alipata elimu yake ya msingi skuli ya Mtakatifu Monika Mkunazini, Zanzibar hadi darasa la nane, Mwaka 1960 hadi 1961 alipata mafunzo ya ualimu kwenye chuo cha ualimu Magila mkoani, Tanga na mwaka 1962 alianza kazi ya kufundisha hadi mwaka 1978.
Akiwa Mwalimu Marehemu Bi. Theresa Olban alikuwa mwana siasa nguli, alianzia tangu kwenye Chama Cha Afro Shirazi (ASP) na baadae Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambako alihudumu nyadhifa mbalimbali ndani CCM na Jumuiya zake kwa kipindi cha maisha yote ya uhai wake.
Mnamo mwaka 1977 hadi 1979 aliwahi kuwa katibu wa CCM tawi la Kwahani na baadae mwaka 1980 aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na Baraza la Wawakilishi, mwaka 1983 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini, Pemba.
Akiwa Mkuu wa Mkoa Kusini, Pemba pia alikua Mjumbe wa Baraza la Chuo cha IDM cha Mzumbe kutoka mwaka 1984 hadi1988, mwaka 1999 hadi 2003 alikuwa Mjumbe wa UWT kwa mkoa wa Mjini Magharibi, awali alianzia na kamati ya Utekelezaji ya UWT Taifa kutoka mwaka 1983 hadi 2003 pia aliwahi kukaimu nafasi ya Katibu Mkuu UWT kwa Zanzibar mwaka 1992 hadi 1995 baadae mwaka 1995 hadi 1999 alikuwa alikuwa Makamu Mwenyekiti UWT Taifa.
Kutoka mwaka 1987 hadi 2002 Marehemu Bi. Thereza Olban aliwahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC)na Mjumbe wa Kamati Maalum ya CCM, Zanzibar. Mwaka 1995 hadi 1988 alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu CCM (CC), mwaka 1980 hadi mwaka 2000, Marehemu Bi. Thereza aliwahi kuwa Mbunge wa Viti maalum wanawake, mwaka 1998 hadi 2002 aliwahi kuwa Mjumbe wa Kamati ya Miradi ya Chama, mwaka 2008 alikuwa Mjumbe wa Baraza la wazee wa CCM Mkoa wa Mjini Magharibi baadae alikuwa Mlezi wa Jumuiya ya Wastaafu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pamoja na utumishi wake wa muda mrefu ndani ya Chama cha CCM, Marehemu Bi. Thereza aliwahi kutunukiwa tunzo ya Utumishi uliotukuka na Rais wa awamu ya saba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Ali Muhamed Shein.Marehemu Bi. Thereza Olban alifariki tarehe 13 Oktoba mwaka huu, ameacha watoto wawili na wajukuu wanne na atazikwa tarehe 15 Oktoba mwaka huu, Mwenyezi Mungu Ailaze roho yake Mahala pema.