RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameeleza kuridhishwa kwa utoaji na usimamizi wa vipaumbele vyote kwa sekta za umma hasa kwa miradi ya kimkakati.Amesema usimamizi huo unalenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma zinazotolewa na kuhakikisha utoaji huduma bora katika maeneo yote ya vipaumbele zikiwemo Elimu, Miundombinu, Uwezeshaji sekta ya Utalii na barabara.

Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo Ikulu Zanzibar, kwenye maadhimisho ya miaka miwili ya Taasisi ya Ofisi ya Rais Ufuatiliaji na Usimamizi wa utandaji Serikalini (ZPDB).Amesema, upatikanaji wa huduma za jamii kwa wakati ni Msingi wa Maendeleo na kigezo muhimu cha utawala bora na uongozi wenye kujali wananchi wake.

Kwa upande mwegine Rais Dk. Mwinyi amezitaka taasisi zote za Serikali kutoa ushirikiano wa kiutendaji kwa maofisa wa taasisi ya ZPDB kwani taasisi hiyo ipo chini yake na kutekeleza juhudu zake za maendeleo.“Kwa uzito wa Taasisi hii,  napenda nieleze kuwa ZPDB ni taasisi iliyopo chini ya Ofisi yangu”. Hivyo, wanapokuja watendaji wa PDB,  mjue nimewatuma mimi na muwape ushirikiano ili kufanikisha utendaji wa kazi zetu” alisisitiza Rais Dk. Mwinyi.

Alisema anataarifa za baadhi ya watendaji na watumishi wa Taasisi za Serikali kwamba hawatoi ushirikiano wa kutosha wa kuiwezesha Taasisi ya ZPDB kutekeleza majukumu yake ipasavyo.Aidha, Dk. Mwinyi ameonya kutotoa ushirikiano kwa taasisi hiyo ni makosa na ameziagiza mamlaka husika kuwachukulia hatua Watendaji na watumishi hao bila ya kumuonea mtu.

Rais Dk. Mwinyi pia ameeleza mafanikio ya ZPDB hayatopatikana bila ya ushirkiano wa kutosha kutoka taasisi nyengine za Serikali hivyo, amezitaka taasisi za umma kwa nafasi zao wana wajibu wa kutekeleza majukumu yao na kuhakikisha nchi inazidi kupiga hatua za haraka za maendeleo katika kukuza uchumi na kuimarisha ustawi wa jamii.

Katika hatua nyengine Rais Dk. Mwinyi ameeleza kufarajika kwake kwa hatua ya ufuatailiaji wa taasisi ya ZPDB hasa kwa sekta za Serikali na kueleza kuwa ufuatiliaji huo unakwenda sambamba na kuanzishwa kwa timu za wataalamu katika Wizara za vipaumbele zitakazosimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa sekta zao.

Alisisititiza kuwa timu ziendelezwe na zijengewe uwezo wa kiutendaji na kitaaluma ili ziongeze ufanisi kwenye utekelezaji wa vipaumbele kwa miradi ya maendeleo.Pia, Rais Dk. Mwinyi ametoa wito kwa wadau wote, zikiwemo Wizara za Serikali, Taasisi binafsi pamoja na washirika wa Maendeleo kuifanyia kazi kauli mbinu ya maadhimisho ya miaka miwili ya PDB inayosema “Ufuatiliaji kwa wakati na usimamizi wa utendaji serekalini ni chachu ya ufanisi, tija ya matokeo ya haraka”  kwa vitendo ili kufanikisha utekelezaji wa vipaumbele vya miradi ya Serikali nchini kwa dhamira na malengo yaliyowekwa yafanikiwe.

Wakati huo huo Rais Dk. Mwinyi amezindua mfumo wa ufuatiliaji   kwa njia ya Kidijitali kwa kutumia “DashBoard” ambapo itarahisisha kwa asilimia kubwa na kuleta ufanisi katika kufuatilia na kutathmini miradi yetu ya maendeleo. Ni matumaini yangu kuwa, sekta zote zitautumia mfumo huo kikamilifu katika utoaji wa taarifa za miradi ya vipaumbele mnayoyatekeleza ili kupata matokeo ya haraka na kuongeza ufanisi unatarajiwa.

ahadi yangu kwa taasisi hii ni kuendelea kuipa ushirikiano kwa kuhakikisha inapatiwa nyezo za kufanyia kazi pamoja na bajeti ya kutosha na kuhakikisha tunashirikiana katika kukabiliana na changamoto ambazo zinapunguza kasi ya utendaji wa taasisi hii katika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi. Nina matumaini makubwa ya kuongeza ufanisi wa Taasisi hii kwa kadri tunavyoendelea mbele na kufikia matarajio ya wananchi wa Zanzibar katika kupiga hatua za maendeleo tunayotarajia.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu, Mhe. Ali Suleiman Ameir ameeleza kuridhishwa kwake na Kasi ya utendaji wa Taasisi ya ZPDB hasa kwa mafanikio makubwa ya Serikali ya Mapindizi ya Zanzibar ya Awamu ya nane.Naye, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Ofisi ya Rais, Ufuatiliaji, Utendaji na Usimamizi Serikalini Zanzibar (ZPDB), Prof. Mohammed Hafidh Khalfan amewashukuru watendaji wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi. Zena Ahmed Said na taasisi nyengine za umma, binafsi na washirika wa Maendeleo kwa michango na ushirikiano mkubwa wanaoutoa kwa taasisi hiyo hadi kufanikiwa kwake kwa kipindi kifupi cha miaka miwili tokea kuasisiwa kwake mwezi Disemba mwaka 2022.

Akizitaja baadhi ya taasisi binafsi zilizosaini makubaliano ya ushirikiano wa kiutendaji na ZPDB Prof. Hafidh ZPDB amezitaja “Zanzibar Maisha Bora Foundation” ZMBF, “Mwanamke Initiative Foundation” (MIF), Tony Blayer Institute, (TBI) ZRA, Azam Marine, Bank za Zanzibar na Tanzania Bara na taasisi nyengine kwa mafanikio makubwa ya ushirikiano hasa kwa sekta ya Elimu ikiwemo kutoa ufadhili wa masomo wa Wananchi wa Zanzibar ndani na nje ya nchi.

Akieleza malengo ya taasisi hiyo, Naibu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Ofisi ya Rais, Ufuatiliaji, Utendaji na Usimamizi Serikalini Zanzibar (ZPDB) Dk. Josephine Kimaro ameleza jukumu kubwa la taasisi hiyo ni kuhakikisha utendaji wa ufanisi kwa kutumia mfumo mpya wa kidijitali wa “DashBoard” utakaowasaidia kuhakikisha kuwepo kwa utamaduni wa utekelezaji kwa Mhe. Rais kwa kumpatia taarifa za uhalisia za kila siku kadri ya utekelezaji unavyoendelea kutoka Wizara za Serikali na taasisi zao kwa sekta mbalimbali zenye miradi ya maendeleo.

Akieleza mafanikio makubwa ya Serikali inayoongozwa na Rais Dk. Mwinyi, Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar, Dk. Muhammed Said Muhammed Dimwa ameshukuru na kupongeza juhudi za Maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mafanikio makubwa aliyoyafanikishwa ndani ya kipindi kifupi cha uongozi wake nakueleza kuwa tayari amefanikisha 150% ya utekelezaji wa Ilani ya chama hicho.

Taasisi ya Ofisi ya Rais, Ufuatiliaji, Utendaji na Usimamizi Serikalini Zanzibar (ZPDB) ilizinduliwa na Rais Dk. Mwinyi mwezi Disemba mwaka 2022, ambayo ilipewa maeneo maalum ya vipaumbele na viashiria ili isimamie.