RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amejumuika na Waumini wa dini ya Kiislamu katika ibada ya sala ya Ijumaa Msikiti wa Maungani Wilaya ya Magharibi B. Akitoa salamu kwa Waumini Alhaj Dk,. Mwinyi amewanasihi Vijana kuwathamini wazazi wao na kuwatendea mema ili kupata baraka za Mwenyezi Mungu.

Alhaj Dk. Mwinyi amefahamisha ni wajibu na ni jambo jema kwa vijana ambao wazazi wao wako hai kuishi nao kwa huruma na upendo na kuwaombea dua wale waliotangulia mbele ya haki kwani kuna fadhila nyingi kwa kutekeleza jambo hilo. Akitoa hotuba ya Ijumaa Khatibu wa Msikiti wa Ijumaa wa Maungani, Sheikh Suleiman Mwinchumu Suleiman amewasisitiza Waumini hao kuwa karibu na wazazi wao pamoja na kuzungumza nao kwa maneno mazuri na kuacha hasira juu yao kama ilivyoamrishwa na miongozo ya dini ya kiislamu.

Katibu Mtendaji wa Afisi ya Mufti, Sheikh Khalid Ali Mfaume amesema ni vyema kwa Waumini wa kiislamu kufahamu du’a ya kuwaombea wazee na kuitekeleza kila wanapopata fursa ya kufanya hivyo, Ili kupata radhi za Mwenyezi Mungu. Wakati huohuo, Alhaj Dk. Mwinyi baada ya sala ya Ijumaa aliendeleza utaratibu wake wa kuwatembelea Wananchi na kuwajulia hali Wagonjwa katika maeneo mbalimbali.

Aliowatembelea leo ni aliekuwa Mbunge na Naibu Waziri Mstaafu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mshauri wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi wa Awamu ya Saba Dk. Maua Abeid Daftari anaeishi Beit Ras Wilaya ya Magharibi A.

Msanii Mkongwe wa sanaa za Filamu na Maigizo Zanzibar Bibi Mwanamwema Khamis Juma, maarufu Bi Njiwa.Mwengine ni Bi. Halima Muhamed, Mjane wa aliekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Kichama, Marehemu Borafya Silima wanaoishi Mwera Mtofaani.