RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewanasihi Waumini wa dini ya Kiislamu kujitathmini na kujua umuhimu wa Ibada kwenye matendo yao ya kila siku.Alhaj Dk. Mwinyi ametoa nasaha hizo leo tarehe 18 Oktoba 2024 alipotoa salamu kwa Waumini hao baada kujumuika nao kwenye ibada ya sala ya Ijumaa, msikiti wa Muhammad Ali, Kidongo Chekundu, Mkoa wa Mjini Magharibi.Ameeleza, ni wajibu wa kila Muumini kuitathmini nafsi yake na anaowaongoza ili kubaini kiasi gani maisha yao yanalingana na Ibada wanazozitekeleza kila siku.
Amesema, kuna mambo mengi yanaendelea ndani ya jamii kwa sababu ya watu kukosa Ucha Mungu(taqwa).Pia Alhajj Dk. Mwinyi ametaja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na Udhalilishaji, ubakaji na Wizi.Aidha, amewahimiza Waumini hao kufanya Ibada kwani Ndio sababu kuu ya kuumbwa kwao.
Akitoa Salamu Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Muft wa Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume amewasisitiza viongozi kuwa mfano bora kwa watu wanaowaongoza kwa kutenda mambo mema.Amewasisitiza Vijana kuacha kushawishika na kujiunga na makundi maovu kwa kisingizio cha dini badala yake kusimamisha sala kwa kuchunga wakati na nidhamu.