RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapindizi Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameitahadharisha jamii kuendelea kuitunza amani na mshikamano uliopo na kuendelea kujenga maendeleo ya nchi.Amesisitiza kuitunza amani hasa wakati wa uchaguzi unapokaribia nchini na kuiasa jamii kutotofautiana na kufarakiana wakati wa uchaguzi mkuu unapofika nchini na kuwataka kuendelea kuwa kitu kimoja.
Al hajj Dk. Mwinyi ametoa nasaha hizo Masjid Hudaa, Machomane Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba alipojumuika na Waumini wa Dini ya Kiislam kwenye Ibada ya sala ya Ijumaa.Amesema, nchi hii inahitaji idumu kwenye amani huku akisisitiza kuwa maendeleo yoyote yana njia ya kufanikiwa kutokana na kuwepo kwa amani, umoja na utulivu na kusisitiza kuwa bila ya nchi kuwa na rasilimali ya amani hakutokuwa na jambo lolote litakalo fanyika na kufanikiwa.
Al hajj Dk. Mwinyi katika kutilia mkazo suala la amani na utulivu ametolea mfano wa mataifa mengine duniani yaliyo kwenye migogoro na kutokuwa na utulivu kwa nchi zao hali aliyoieleza kuathiri maendeleo ya nchi zao ikiwemo uchumi kutetereka.Akizungumza kwenye ibada ya sala hiyo, Katibu Mtendaji kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume amesema, amani haivunjiki kwa siku moja bali huanza kwa uchochezi wa maneno na vitendo miongoni mwa jamii kwa kujibizana na kupigana hali inayokwamisha maendeleo na kushuka kwa uchumi wa nchi.
Kwa upande mwengine Al hajj Dk. Mwinyi pia amehudhuria du’a maalumu ya kuiombea nchi kuendelea kuwa katika hali ya amani, umoja na utulivu ambayo iliandaliwa na Ofisi ya Mufti Zanzibar, ilifanyika Masjid Rahman, Gombani Mpya, Mkoa wa Kusini Pemba. Dua hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Chama Cha Mapinduzi pamoja na Wananchi wa mikoa yote ya Kusini na Kaskazini, Pemba.