RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza mikakati inayochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kupambana na maradhi mbali mbali yakiwemo ya miripuko ambapo yanapozuka huathiri watu wa rika zote wakiwemo watoto.
Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo ya Watoto (UNICEF) nchini Tanzania Maniza Zaman aliyefuatana na Mkuu mpya wa Shirika hilo hapa Zanzibar Maha Damaj ambaye alifika kujitambulisha kwa Rais.
Rais Dk. Shein alieleza kuwa miongoni mwa juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hivi sasa ni pamoja na kujenga mitaro mikubwa katika eneo la mji wa Zanzibar ambayo matokeo yake itaisadia kuondosha matuamo ya maji ambayo hatimae huleta maradhi ya miripuko na kulata athari kubwa kwa jamii.
Aliongeza kuwa katika kipindi kifupi ambacho bado mradi huo ujenzi wake unaendelea tayari mradi umeanza kuleta matumaini makubwa ambapo athari mbali mbali ambazo hapo siku za nyuma zilikuwa zikitokea zimepungua ikiwemo kutuama kwa maji pamoja na kuleta mafuriko.
Aidha, Rais Dk. Shein alieleza kuwa mbali ya jitihada hizo suala zima la elimu pamoja na kuendeleza Sera na mikakati ya Serikali katika kupambana na maradhi mbali mbali pamoja na kuimarisha ustawi wa akina mama na watoto zimekua zikichukuliwa.
Hata hivyo, Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kulipongeza Shirika la UNICEF kwa jitihada zake za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuhakikisha watoto wa Zanzibar wanapata haki zao za msingi ikiwa ni pamoja na elimu, afya pamoja na huduma nyengine za kijamii.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa kuwepo kwa Programu ya Pamoja ya Zanzibar” (ZIP), inayohusisha Mashirika tisa ya UN iliyozinduliwa hivi karibuni kutasaida katika kuleta mafanikio yaliokusudiwa kwa wananchi wa Zanzibar.
Nae Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia Watoto Duniani (UNICEF) nchini Tanzania Bi Maniza Zamani alipongeza juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika suala zima la kuwahudumia watoto pamoja na akina mama.
Bi Zamani alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweza kupata mafanikio makubwa katika kuwahudumia watoto sambamba na kuhakikisha wanapata haki zao za msingi ikiwemo kupata elimu na afya bora huku akizipongeza juhudi za Serikali.
Alieleza kuwa Shirika hilo linathamini juhudi hizo na limeweza kushuhudia mafanikio na mabadiliko makubwa katika sekta za maendeleo hatua ambazo zimewawezesha watoto wa Zanzibar kuweza kupata haki zao za msingi pamoja na mahitaji yao muhimu ya kimaisha.
Mwakilishi huyo alieleza azma ya programu ya pamoja ya UN hapa Zanzibar kuwa mbali na mambo mengine pia, itasaidia kupunguza vifo vya uzazi, ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Aliongeza kuwa Shirika la (UNICEF) limekwua likichukua juhudi zake katika kuhakikisha wananchi wa ngazi ya chini katika jamii wanashirikishwa kwa kuweka Kamati ndogondogo katika jamii katika kuhakikisha inakwenda sambamba na mikakati iliyowekwa na Shirika hilo.
Wakati huo huo, Rais Dk. Shein alikutana na Dk. Tigest Ketsela Mengestu, Mwakilishi Mkaazi mpya wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Tanzania na kulipongeza Shirika hilo kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar.
Rais Dk. Shein alieleza kuwa Shirika la (WHO),lina historia ya miaka mingi katika kuiuinga mkono na kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kusaidia katika maradhi mbali mbali yakiwemo Kipindupindu yalivyotokea hapo siku za nyuma katika historia ya Zanzibar.
Alieleza kuwa mbali ya maradhi hayo, (WHO) imekuwa ikisaidia kwa kiasi kikubwa katika kukabiliana na maradhi mbali mbali pamoja na kushirikiana na Zanzibar katika kuwasomesha wataalamu wa afya.
Pia, Rais Dk. Shein alisisitiza haja kwa Shirika hilo la (WHO) kuendelea kufanya kazi na Wizara ya Afya huku akiahidi kuwa Serikali anayoiongoza itaendelea kushirikiana na viongozi hao wote wapya wa Mashirika ya (UN) watakaofanya kazi za hapa nchini.
Nae Dk. Tigest Ketsela Mengestu, ambaye alifika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha kwa Rais wa Zanzibar alipongeza juhudi za Serikali ya Mapinduzi chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein katika kuimarisha sekta ya afya na kuahidi kuwa Shirika la (WHO) litaendelea kuisadia na kuiunga mkono Zanzibar.
Kadhalika, Dk. Mangestu alimpongeza Rais Dk. Shein kwa juhudi zilizochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi katika kuhakikisha mapambano ya maradhi ya Malaria yanapungua na kuondoka kabisa katika visiwa vya Zanzibar na kuwa kigezo kwa nchi nyengine duniani.