Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi ameondoka nchini kuelekea Doha,Qatar ambapo anatarajia kushiriki katika Mkutano wa Kimataifa wa kutimia miaka Thelathini ya Familia Duniani utakaofanyika tarehe 29 hadi 31 Oktoba 2024 nchini Humo.Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hamad Rais Dk.Mwinyi na ujumbe wake amepokelewa na viongozi waandamizi wa Qatar wakiongozwa Mhe. Youssef Al Harami na Balozi wa Tanzania nchini Qatar,Balozi Habibu Awesi Mohamed.
Ushiriki wa Rais Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi katika Mkutano huo mkubwa wa Kimataifa utaongeza chachu ya Ustawi wa Maendeleo ya Wananchi wa visiwa vya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.Hii ni mara ya tatu Mhe.Rais Dk.Hussein Ali Mwinyi kuizuru Qatar akiwa katika kipindi chake cha Urais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi leo katika siku ya kwanza ya ziara yake nchini Qatar ambapo mapema asubuhi alikutana na Waziri wa nchi wa Qatar anayeshughulikia masuala ya Nishati Mheshimiwa Saad bin Sherida Al- Kaabi.Mazungumzo hayo yametoa nuru kwa Qatar kuiuzia Tanzania mbolea aina ya Urea kwa gharama nafuu.
Mazungumzo hayo alihudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania nchini Qatar Mheshimiwa Habib Awesi Mohammed pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mbolea ( TFC ) Samwel Ahadi Mshote.Kesho akimaliza ziara yake nchini Qatar Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi anatarajiwa kushiriki mkutano mkubwa wa Kimataifa wa kutimiza miaka 30 ya Familia Duniani utakaofanyika jijini Doha.
Mkutano huo unafuatia Azimio la mwaka 1994 la Umoja wa Mataifa la Mwaka wa Kimataifa wa Familia ( IYF ) lililopitishwa rasmi na Baraza la Umoja wa Mataifa likizingatia thamani na umuhimu uliopo wa kuzilinda na kuzisaidia familia kupitia sheria za Kimataifa.Maazimio ya mwaka wa Kimataifa wa Familia hufanyika kila baada ya miaka kumi.